Sera za uchumaji mapato kwenye chaneli za YouTube

Unapotumia muziki uliozalishwa na Dream Track katika video ndefu, video yako haitachuma mapato kupitia matangazo au ugavi wa mapato yanayotokana na usajili (YouTube Premium).

Tarehe 10 Machi, 2022: Kutokana na kusimamishwa kwa mifumo ya utangazaji ya Google hivi majuzi nchini Urusi, tutasitisha ufunguaji wa akaunti mpya za Urusi kwenye AdSense, AdSense katika YouTube, AdMob na Google Ad Manager. Pia, tutasitisha matangazo kwenye Huduma na mitandao ya Google kwa ujumla kwa watangazaji wanaoishi nchini Urusi. Kwa hivyo, watayarishi nchini Urusi hawataweza kujisajili kwenye Mpango wa Washirika wa YouTube kwa sasa.

Tarehe 3 Machi 2022: Kutokana na vita vinavyoendelea nchini Ukraini, tutasitisha kuonyesha kwa muda matangazo ya Google na YouTube kwa watumiaji wanaoishi nchini Urusi. Pia, tunasitisha uwezo wa kufikia vipengele vyote vya uchumaji wa mapato (kama vile Uanachama katika chaneli, Super Chat, Super Stickers, na Bidhaa) kwa watazamaji wanaoishi nchini Urusi. Pata maelezo zaidi

Tarehe 25 Februari 2022: Kutokana na hali ya vita nchini Ukraini, tunasitisha uchumaji wa mapato kwenye YouTube kwa chaneli za habari zinazofadhiliwa na serikali ya Urusi. 

Tutaendelea kufuatilia hali kwa ukaribu na kufanya marekebisho ipasavyo.

Imesasishwa Aprili 2024: Lugha katika sera zetu za mpango imesasishwa ili kufafanua maana ya maudhui Yanayojirudia na Yanayotumiwa tena ya watayarishi. Sera zetu za maudhui Yanayojirudia na Yanayotumiwa tena hazijabadilika.

Ikiwa unachuma mapato kwenye YouTube, ni muhimu chaneli yako ifuate sera za uchumaji wa mapato kwenye YouTube. Sera hizo zinajumuisha zilizofafanuliwa hapo chini pamoja na Mwongozo wa Jumuiya ya YouTube, Sheria na Masharti, Hakimiliki, Sera za Marekebisho ya Kuidhinisha Haki na  Sera zetu za mpango.

Sera hizi zinatumika kwa mtu yeyote ambaye tayari amejiunga au anayefikiria kuomba kujiunga kwenye Mpango wa Washirika wa YouTube. Pia, sera za uchumaji wa mapato kwenye Video Fupi za YouTube hutumika ikiwa unachuma mapato kwenye Video Fupi katika YouTube.

Ni lazima maudhui yote yanayochuma mapato kupitia matangazo yafuate mwongozo wetu wa maudhui yanayofaa watangazaji. Ili kuchuma mapato kupitia vipengele vya ufadhili kutoka kwa mashabiki, ni lazima watumiaji wa mara ya kwanza wakubali masharti ya Sehemu ya Bidhaa za Biashara (CPM) kabla ya kuwasha vipengele mahususi. Ni lazima pia ufuate sera za uchumaji mapato kwenye Bidhaa za Biashara unapochuma mapato kupitia vipengele vya ufadhili kutoka kwa mashabiki.

Ufuatao ni muhtasari mfupi wa kila sera kuu. Hakikisha unasoma kila sera kwa kina, kwa kuwa sera hizi zinatumika kukagua ikiwa chaneli inatimiza masharti ya kuchuma mapato. Wahakiki wetu hukagua mara kwa mara ili kuona ikiwa chaneli zinazochuma mapato zinafuata sera hizi. Pata maelezo zaidi kuhusu jinsi tunavyotekeleza sera zetu.

Kumbuka kuwa tunapotumia neno video kwenye ukurasa huu, tunarejelea Video Fupi, video ndefu na utiririshaji mubashara. Sera hizi zinatumika katika sehemu zozote ambapo video hutazamwa ikiwa ni pamoja na Ukurasa wa kutazama (kurasa katika YouTube, YouTube Music au YouTube Kids), Kicheza Video cha YouTube (kichezaji kinachopachika maudhui ya YouTube kwenye tovuti nyingine) na Kicheza Video Fupi za YouTube (kichezaji kinachofanya Video Fupi zipatikane).

Vitu tunavyoangalia tunapokagua chaneli yako

Ikiwa unachuma mapato kwenye YouTube, maudhui yako ni lazima yawe asili na yenye uhalisia. Hii inamaanisha kuwa tunatarajia maudhui yako: 

  • Yatokane na ubunifu wako asili. Ukitumia maudhui ya mtu mwingine, unapaswa uyabadilishe kwa namna inayofaa ili uyatumie kama maudhui yako.
  • Yasiwe ya kunakili wala yasijirudie. Maudhui yako yanapaswa kutayarishwa kwa lengo la kufurahisha au kuelimisha watazamaji, badala ya lengo kuwa kupata utazamaji pekee. 

Wahakiki wetu watakagua chaneli na maudhui yako kulingana na sera zetu. Kwa sababu hawawezi kukagua kila video, huenda wahakiki wetu wakazingatia zaidi mambo yafuatayo kwenye chaneli yako:

  • Mada kuu
  • Video zilizotazamwa zaidi
  • Video mpya
  • Kiwango cha juu cha muda wa kutazama
  • Metadata ya video (ikiwa ni pamoja na majina ya video, vijipicha na maelezo)
  • Sehemu ya “Kuhusu” ya chaneli

Hii ni mifano tu ya baadhi ya vipengele ambavyo wahakiki wetu wanaweza kutathmini. Kumbuka kuwa wahakiki wetu wanaweza kukagua sehemu nyingine za chaneli yako ili kuona iwapo inafuata sera zetu kikamilifu.

Kufuatilia Mwongozo wa Jumuiya ya YouTube

Mwongozo huu husaidia YouTube kuendelea kuwa jumuiya bora kwa watazamaji, watayarishi na watangazaji. Mtu yeyote katika YouTube anafaa kufuata Mwongozo wetu wa Jumuiya na maudhui yoyote unayochapisha ni lazima yafuate kikamilifu Mwongozo wetu wa Jumuiya.

Watayarishi wanaochuma mapato wanapaswa kufahamu kwamba mwongozo huu utatumika si tu kwa kila video, lakini pia kwa chaneli yako kwa ujumla. Maudhui yanayokiuka Mwongozo wa Jumuiya ya YouTube hayakidhi vigezo vya kuchuma mapato na yataondolewa katika YouTube.
Kufuata sera zetu za mpango
AdSense katika YouTube huwawezesha washirika wa YouTube kulipwa kwa video zao zinazochuma mapato. Hakikisha unafuata sera zetu za mpango na Sheria na Masharti ya YouTube.

Maudhui yanayojirudia

Maudhui yanayojirudia hurejelea chaneli ambayo maudhui yanalingana sana kiasi kwamba watazamaji wanaweza kutatizika kubaini tofauti kati ya video. Hii hujumuisha maudhui yanaoonekana kuwa yametayarishwa na kiolezo ambacho hakijabadilishwa au kimebadilishwa kidogo kwenye video zote au maudhui yanayoweza kuigwa kwa urahisi.

Sera hii inatumika kwa chaneli yako kwa ujumla. Yaani, iwapo una video nyingi zinazokiuka mwongozo wetu, uchumaji wa mapato unaweza kuondolewa kwenye chaneli yako yote.

Maudhui yanayoruhusiwa kuchuma mapato

Sera hii inahakikisha kuwa maudhui yanayochuma mapato yanawapa watazamaji kitu kinachofurahisha na kinachovutia kutazama. Kwa maneno mengine, ikiwa mtazamaji wa kawaida anaweza kubainisha kuwa maudhui ya chaneli yako hutofautiana kati ya video moja na nyingine, basi yanafaa kuchuma mapato. Tunafahamu kuwa chaneli nyingi hutayarisha maudhui yanayofuata mtindo unaofanana. Kilicho muhimu ni kwamba, maudhui na ubunifu wa kila video ni lazima vitofautiane kiasi.

Mifano ya maudhui yanayoruhusiwa kuchuma mapato (ni pamoja na, lakini si tu):

  • Utangulizi na utamatishaji unaofanana katika video zako, lakini sehemu kubwa ya maudhui yako ni tofauti
  • Maudhui yanayofanana, ambapo kila video inajadili kwa upekee kuhusu sifa za mada unayoangazia
  • Klipu fupi za vipengee vinavyofanana zilizohaririwa pamoja ambapo unaelezea jinsi zinavyohusiana

Maudhui yanayokiuka mwongozo huu

Maudhui ya chaneli yanapojumuisha maudhui yanayofanana, yanaweza kuwachukiza watazamaji ambao wanatumia YouTube ili kuona video zinazofurahisha na kuvutia. Hii inamaanisha kuwa chaneli zilizo na maudhui yenye utofauti mdogo kati ya video haziruhusiwi kuchuma mapato. Kwa maneno mengine, chaneli yako haipaswi kuwa na maudhui yaliyotayarishwa kwa kutumia kiolezo na kurudiwa kwa kiwango kikubwa.

Mifano ya maudhui ambayo hayapaswi kuchuma mapato (orodha hii haijakamilika):

  • Maudhui yanayoangazia kwa upekee usomaji wa maudhui mengine ambayo hukuyabuni, kama vile maandishi kutoka kwenye tovuti au mipasho ya habari
  • Nyimbo zilizobadilishwa ili kugeuza sauti au kasi, lakini zinafanana na wimbo wa asili
  • Maudhui yanayofanana, yanayorudiwa au maudhui ya ovyo yenye thamani ndogo ya maoni, masimulizi au mafunzo
  • Maudhui yanayotayarishwa kwa wingi au yanayotumia kiolezo kinachofanana kwenye video mbalimbali
  • Maonyesho ya slaidi za picha au maandishi ya kusogezwa yaliyo na thamani ndogo au yasiyo na thamani yoyote ya maoni, masimulizi au mafunzo

Maudhui ambayo yametumika tena

Maudhui ambayo yametumika tena yanarejelea chaneli ambazo hubadilisha maudhui ambayo tayari yapo kwenye YouTube au chanzo kingine cha mtandaoni bila kuongeza maoni halisi, maboresho muhimu au thamani ya mafunzo au burudani. Maudhui ambayo yametumika tena yanaweza pia kutambulika kuwa maudhui yanayorudiwa au yaliyokusanywa kutokana na maudhui ya wengine (kuchukua maudhui asili au ya kipekee kwenye tovuti nyingine na kuyachapisha kama yako). 

Ili kubaini ikiwa maudhui yako yametumika tena, wahakiki wetu watakagua chaneli yako ili kufahamu jinsi ulivyotayarisha, ulivyoshiriki au kuchapisha maudhui yako. Wahakiki wetu wanaweza kukagua mambo yafuatayo kwenye chaneli yako: 

  • Video 
  • Maelezo ya chaneli
  • Jina la video
  • Maelezo ya video

Sera yetu ya maudhui ambayo yametumika tena inatumika kwenye chaneli yako kwa ujumla. Endapo una video zinazokiuka mwongozo wetu au ikiwa hatuwezi kubaini kwa usahihi iwapo ulitayarisha maudhui, uchumaji mapato unaweza kuondolewa kwenye chaneli yako nzima.

Maudhui yanayoruhusiwa kuchuma mapato

Tungependa kuwalipa watayarishi kwa maudhui asili na yenye uhalisia, yanayoongeza thamani kwa watazamaji. Ukiweka kichekesho au ubunifu kwenye maudhui ambayo hukutayarisha hapo awali (kwa kuzingatia mwongozo wetu hapo chini), utakuwa umebadilisha maudhui kwa kiasi fulani. Ni sawa kuwa na aina hii ya maudhui kwenye chaneli yako, lakini video husika zinaweza kutegemea sera nyingine kama vile hakimiliki. Kwa maneno mengine, tunaruhusu maudhui ambayo yametumika tena ikiwa watazamaji watabaini kuwa kuna utofauti unaovutia kati ya video asili na video yako.

Kumbuka: Ingawa mifano hii haikiuki sera ya kuchuma mapato kwenye maudhui ambayo yametumika tena, sera nyingine, kama vile hakimiliki, bado zinatumika.

Mifano ya maudhui yanayoruhusiwa kuchuma mapato (ni pamoja na, lakini si tu):

  • Kutumia klipu kutoa maoni muhimu
  • Tukio ulilolitoa kwenye filamu ambalo umeliandikia upya mazungumzo na kubadilisha sauti
  • Kucheza tena mashindano ya spoti ambako unaelezea mambo yaliyofanya mchezaji ashinde
  • Video za maoni ambako unatoa maoni kuhusu video asili
  • Video iliyohaririwa kutoka kwa watayarishi wengine ambako unaweka hadithi na maoni
  • Uhariri wa maudhui mseto katika Video Fupi kama vile kuweka maudhui asili kwenye wimbo katika maktaba yetu au kuweka sehemu ya sauti au video asili kutoka kwenye video nyingine katika maudhui yako
  • Maudhui yanayomwangazia mtayarishi aliyepakia maudhui katika video
  • Maudhui ambayo yametumika tena kutoka kwenye vyanzo vingine vya mtandaoni ambapo mtayarishi anaonekana kwenye maudhui au yanafafanua jinsi mtayarishi alivyoyaongeza kwenye maudhui
  • Video iliyohaririwa yenye madoido ya sauti au video juu ya maudhui ya video ambayo yametumika tena inayoonyesha uhariri wa kina na kuwa ni ya kipekee kwenye chaneli yako

Maudhui yanayokiuka mwongozo huu

Kuchukua maudhui ya mtu mwingine, kufanya mabadiliko machache na kuyaita maudhui hayo kuwa yako kutakuwa ukiukaji wa mwongozo huu. Ikiwa tutashindwa kubaini kuwa maudhui ni yako, yatashughulikiwa kulingana na sera yetu ya maudhui ambayo yametumika tena. Sera hii hutumika hata kama umepewa idhini na mtayarishi wa maudhui halisi. Maudhui ambayo yametumika tena ni tofauti na utekelezaji wa YouTube wa Hakimiliki, kumaanisha kuwa maudhui hayo hayapo chini ya hakimiliki, ruhusa au matumizi ya haki. Mwongozo huu unaamanisha kuwa wakati mwingine, huenda usipate madai dhidi ya maudhui yako, lakini chaneli yako bado inaweza kuwa imekiuka mwongozo wetu wa maudhui ambayo yametumika tena.

Mifano zaidi ya maudhui ambayo hayapaswi kuchuma mapato (orodha hii haijakamilika):

  • Klipu za matukio kutoka kwenye kipindi ukipendacho zilizohaririwa pamoja, zikiwa na thamani ndogo au bila thamani yoyote ya masimulizi
  • Video fupi ulizokusanya kutoka kwenye tovuti nyingine za mitandao ya kijamii
  • Mikusanyiko ya nyimbo kutoka kwa wasanii tofauti (hata kama wamekuruhusu)
  • Maudhui yaliyopakiwa mara nyingi na watayarishi wengine
  • Kutangaza maudhui ya watu wengine (hata kama wamekuruhusu)
  • Maudhui yaliyopakuliwa au kunakiliwa kutoka kwenye chanzo kingine cha mtandaoni bila marekebisho yoyote ya muhimu 
  • Maudhui yanayotazamwa kutokana na miitikio isiyo ya maneno kwenye video zako bila maoni ya sauti
Kanuni za ubora wa maudhui ya watoto na familia
Lengo letu ni kuwapa watoto na familia hali bora na salama ya utumiaji kwenye YouTube, huku tukitafuta mbinu mpya za kuwalipa watayarishi wanaochangia maudhui yaliyo na ubora wa juu kwenye mfumo.

Ikiwa chaneli yako ina maudhui “yanayolenga watoto”, tutatumia kanuni za ubora wa maudhui ya watoto na familia kwenye YouTube ili kubaini hali ya uchumaji mapato ya maudhui hayo.

Iwapo chaneli itapatikana inaangazia sana maudhui ya ubora wa chini “yanayolenga watoto”, inaweza kusimamishwa kwenye Mpango wa Washirika wa YouTube. Iwapo video mahususi itapatikana kuwa inakiuka kanuni hizi za ubora, inaweza kupata matangazo machache au isipate kabisa.

Unapokagua ili uone ikiwa maudhui yako ya “yanayolenga watoto” yana ubora wa chini au wa juu, kigezo cha muktadha na utofauti ni muhimu. Tembelea ukurasa wetu wa mbinu bora za kutayarisha maudhui ya watoto na familia ili upate mwongozo na mifano.

Kutumia kanuni za ubora kubaini utimizaji wa masharti ya kuchuma mapato

Kuna kanuni kadhaa kuhusu maudhui ya ubora wa chini zinazoweza kuathiri ubora wa jumla wa video husika. Tutazingatia kila kanuni kama kigezo cha kutimiza masharti ya kuchuma mapato hatua kwa hatua. Kwa sasa tunatekeleza kanuni zilizoorodheshwa hapo chini dhidi ya ubora wa chini kwa maudhui ya watoto na familia. Tunaweza kuongeza upeo ili kujumuisha kanuni zaidi za ubora kadiri muda unavyosonga.

  • Kuhimiza tabia au mitazamo hasi: Maudhui yanayohimiza shughuli hatari, ubadhirifu, uchokozi, udanganyifu au kuwakosea wengine heshima (k.m. mizaha isiyo salama na hatari, ulaji usiofaa).
  • Yanayolenga kutangaza biashara au ofa kwa kiasi kikubwa: Maudhui ambayo yanalenga zaidi ununuzi wa bidhaa au kukuza chapa na nembo (k.m. vifaa vya watoto kuchezea na chakula). Pia, inajumuisha maudhui yanayolenga ununuzi wa bidhaa kupita kiasi. Pata maelezo zaidi kuhusu maudhui yaliyo na matukio mengi ya kibiashara kwenye YouTube Kids.
  • Mafunzo yanayopotosha: Maudhui yanayodai kuwa ya mafunzo katika sehemu ya kichwa au kijipicha chake, lakini hayana mwongozo au maelezo au hayafai kutazamwa na watoto. Kwa mfano, vichwa au vijipicha ambavyo vinaahidi kuwasaidia watazamaji “kujifunza rangi” au “kujifunza namba,” lakini badala yake video inaelezea maelezo yasiyo sahihi.
  • Maudhui yasiyoeleweka: Maudhui yasiyojitosheleza, yenye masimulizi yasiyooana au yasiyoeleweka kama vile kuwa na sauti isiyosikika. Aina hii ya video mara nyingi hutokana na uandaaji wa maudhui mengi kwa pamoja au utayarishaji wa kiotomatiki.
  • Maudhui yanayoshtua au yanayopotosha: Maudhui ambayo si ya kweli, yaliyotiwa chumvi, ya ajabu au yanayotokana na maoni na yanayoweza kuchanganya hadhira ya watoto. Yanaweza pia kujumuisha “uwekaji wa maneno muhimu”, au matumizi ya maneno muhimu maarufu ya kuvutia watoto kwa kurudiwa, kubadilishwa au kutiwa chumvi. Maneno muhimu yanaweza pia kutumika katika njia isiyo na maana.
Wajibu wa mtayarishi
Mafanikio ya chaneli yako na Mpango wa Washirika wa YouTube yanategemea utayari wa watangazaji kuhusisha chapa zao na maudhui ya YouTube. Watangazaji wanapopoteza imani, mapato ya watayarishi wote wa YouTube huathiriwa vibaya.
Haturuhusu tabia mbaya ambayo ina athari kubwa kwa jumuiya. Sera hii inamaanisha kuwa unapaswa kuwaheshimu watazamaji wako, watayarishi wenzako na watangazaji wetu, ndani na nje ya YouTube.
Ukikiuka sera hii, tunaweza kuzima kwa muda uchumaji wa mapato au kusimamisha akaunti zako. Hatua hii inaweza kutumika katika chaneli zako zote zilizopo na chaneli zozote mpya unavyoanzisha pamoja na chaneli ambako unaangaziwa mara kwa mara.
Iwapo chaneli zako zozote zimekomeshwa kuchuma mapato au kusimamishwa, hupaswi kuanzisha chaneli mpya (au kutumia chaneli zilizopo) ili kukwepa masharti haya au kutuma maombi ya kujumuishwa kwenye Mpango wa Washirika wa YouTube kupitia chaneli zinazohusiana wakati wa kipindi chako cha kusimamishwa. Kufanya hivyo kunaweza kusasabisha kusimamishwa kwa chaneli zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu Wajibu wa mtayarishi.
Uadilifu wa mtayarishi

Tunatarajia kwamba watayarishi walio kwenye Mpango wa Washirika wa YouTube watafanya shughuli zao kulingana na maelezo waliyoyatoa na si kutumia uwakilishi wa uongo kwa kuvuruga shughuli zao kwenye mfumo au kujihusisha na tabia za udanganyifu.

Hii ina maana kwamba watayarishi hawapaswi kuongeza kwa njia bandia ushirikishaji wa chaneli, kama vile mara za kutazamwa, wanaofuatilia, alama za kupendwa, muda wa kutazama na maonyesho ya matangazo. Pia, watayarishi hawapaswi kuhamasisha ushiriki wa hiari kwenye maudhui yasiyotii masharti kabla ya kufuta au kuficha maudhui hayo. Kujihusisha na tabia ya aina hii huenda kukapelekea uondolewe kwenye Mpango wa Washirika wa YouTube au kusimamishwa kwa chaneli zako. Angalia sera zetu za mpango ili upate maelezo zaidi

Pia, watayarishi hawapaswi kuwapotosha watumiaji au YouTube kwa kushiriki katika matumizi mabaya ya kifedha, kama vile kutumia vipengele vyetu vya uchumaji wa mapato kwa miamala isiyo halali, ya ulaghai au danganyifu. Ukikiuka sera hii, huenda tukakuondoa kwenye Mpango wa Washirika wa YouTube au kusimamisha chaneli yako.

Jinsi tutakavyokutaarifu kuhusu mabadiliko ya sera

YouTube hubadilisha na kuboresha Huduma mara kwa mara, ili kuendana na ulimwengu unaotuzunguka. Huenda tukahitaji kubadilisha sheria na masharti au sera zinazotumika kwenye utumiaji wako wa Huduma - ikiwa ni pamoja na Sheria na Masharti, na Sheria na Masharti ya Mpango wa Washirika wa YouTube, sera zetu na hati nyingine za kimkataba - ili kujumuisha mabadiliko yaliyofanyika kwenye Huduma zetu au kwa sababu za kisheria, kanuni au usalama.

Tutakujulisha kwa maandishi tutakapofanya mabadiliko yanayoweza kukuathiri. Ikiwa hukubali marekebisho ya sheria na masharti, unaweza kuacha kutumia kipengele husika au kusimamisha makubaliano yako nasi.

Ili kukusaidia uendelee kufahamu yanayoendelea kuhusu sera zetu, pia tunadumisha kumbukumbu ya kudumu ya masasisho. Angalia hapa orodha yetu ya mabadiliko.

Jinsi tunavyotekeleza sera za uchumaji wa mapato kwenye YouTube

Yeyote anayepata pesa kwenye YouTube ni lazima afuate sera za uchumaji wa mapato za chaneli za YouTube. Ukikiuka sera yetu yoyote, YouTube inaweza ikakuchukulia hatua zilizobainishwa hapa chini.

Kuzuia, kurekebisha, kutoza au kukata mapato au malipo

Tunaweza tukazuia au tukarekebisha mapato yako yoyote yanayohusishwa na ukiukaji wa sera za uchumaji mapato kwenye Chaneli za YouTube. Pia, tunaweza tukatoza mapato yanayohusiana kwenye salio lolote la AdSense katika YouTube ambalo hujalipwa au kukata kiasi hicho kwenye mapato utakayolipwa baadaye.

Kwa ukiukaji wowote kama huo, tunahitaji muda wa kuchunguza ikiwa mapato yanahitaji kuzuiwa, kurekebishwa au kukatwa. Hali hii inaweza kusababisha kucheleweshwa kwa malipo kwa hadi siku 90 au hadi tutakaposuluhisha mizozo yoyote ya haki za wahusika wengine.

Mifano ya ukiukaji ambao huenda ukafanya tukazuia au kurekebisha mapato yako inajumuisha (lakini si tu) matukio ya:

Iwapo chaneli yako imefungwa au imesimamishwa kwenye Mpango wa Washirika wa YouTube, hustahiki tena kuchuma mapato yoyote. Huenda pia YouTube ikazuia mapato na kuwarejeshea watangazaji au watazamaji pesa walizotumia kwa ununuzi, inapofaa na inapowezekana.

Tutakujulisha kwa barua pepe au ndani ya bidhaa pindi tunapohitaji kutekeleza sera zetu. Pia, tutakujulisha kuhusu njia za utatuzi unazoweza kutumia.

Kuweka kikomo cha mapato ya matangazo kwenye video zako

Kama mshirika wa Mpango wa Washirika wa YouTube, unaweza kufanya video zako zitimize vigezo vya kuchuma mapato ya matangazo ikiwa zinatii mwongozo wetu wa maudhui yanayofaa watangazaji. Hata hivyo, ikiwa video zako zitapatikana kuwa hazitimizi mwongozo wetu wa maudhui yanayofaa watangazaji au ikiwa zinakiuka sera nyingine, kama vile mipaka yetu ya umri au mwongozo wa hakimiliki, video zako zinaweza kuchuma mapato machache ya matangazo au zikakosa kuchuma mapato kabisa.

Kwa maelezo zaidi kuhusu sababu zinazoweza kufanya maudhui yasitimize masharti ya kuchuma mapato, angalia: Mwongozo wa aikoni ya uchumaji wa mapato kwenye Studio ya YouTube

Kusimamisha ushiriki wako kwenye Mpango wa Washirika wa YouTube

Ukiukaji wa sera za uchumaji wa mapato kwenye chaneli za YouTube unaweza kusababisha uchumaji wa mapato usimamishwe au ufungwe kabisa kwenye baadhi au akaunti zako zote. Ikibainishwa kuwa chaneli yako haitimizi tena masharti ya mpango wa uchumaji wa mapato, chaneli yako inaweza kupoteza uwezo wa kufikia vipengele na zana zote za uchumaji wa mapato pamoja na Sehemu zinazohusiana na Mpango wa Washirika wa YouTube. Pia, unaweza kujiondoa kwenye baadhi ya Sehemu mahususi za uchumaji wa mapato wakati wowote kwa kuwasiliana na Usaidizi kwa Watayarishi.

Kuhifadhi data

Makubaliano ya uchumaji wa mapato kati yako na YouTube yakisimamishwa, bado unaweza kuomba data ya Takwimu za YouTube za tangu wakati ulipokuwa kwenye mpango kwa kuwasiliana na huduma ya Usaidizi kwa Watayarishi.

Ili upate maelezo zaidi kuhusu kusimamishwa, ikiwa ni pamoja na vidokezo vya utatuzi na maelezo kuhusu jinsi ya kuomba kujiunga tena na mpango, angalia: Uchumaji wa mapato umezimwa kwenye chaneli yangu

Kusimamisha au hata kufunga chaneli yako ya YouTube

Katika hali za kipekee tunaweza kuhitaji kusimamisha chaneli, akaunti au kuzima uwezo wa mtumiaji kufikia Huduma ili kulinda uadilifu wa mfumo au kuwalinda watumiaji wetu dhidi ya hatari. Pata maelezo zaidi kuhusu kusimamishwa kwa chaneli na akaunti za Google zilizozimwa pamoja na hatua unayoweza kuchukua iwapo unaamini kuwa chaneli au akaunti yako ilisimamishwa kimakosa.

Jinsi tutakavyokutaarifu kuhusu vitendo vinavyoathiri uchumaji wako wa mapato

Tutakujulisha kwa barua pepe au ndani ya bidhaa pindi tunapohitaji kutekeleza sera zetu. Pia, tutakujulisha kuhusu njia za utatuzi unazoweza kutumia.

Jinsi ya kupata usaidizi wa matatizo yanayokuathiri

Ikiwa upo kwenye Mpango wa Washirika wa YouTube, unaweza kuwasiliana na timu yetu ya Usaidizi kwa Watayarishi.

Iwe unakabiliwa na tatizo mahususi au unataka kujua jinsi ya kunufaika zaidi na YouTube kama mtayarishi, tuko hapa kukusaidia:

  • Kuboresha jinsi unavyotumia YouTube
  • Kufahamu jinsi ya kunufaika zaidi na Zana zetu za takwimu
  • Kupata vidokezo kuhusu vipengele vya kiufundi au huduma za YouTube
  • Kupata maelezo kuhusu jinsi ya kutii sera na mwongozo wa hakimiliki
  • Kupata majibu ya maswali kuhusu usimamizi wa akaunti na chaneli
  • Kusuluhisha matatizo ya usimamizi wa haki na Content ID
  • Kutatua na kurekebisha hitilafu au matatizo ya akaunti yako

Unaweza kupata maagizo ya kina kuhusu jinsi ya kuwasiliana na huduma ya Usaidizi kwa Watayarishi na jinsi ya kupata usaidizi ukiwa Mtayarishi wa YouTube.

Je, maelezo haya yamekufaa?

Tunawezaje kuboresha?
Tafuta
Futa utafutaji
Funga kisanduku cha kutafutia
Menyu kuu
17950045056606273295
true
Tafuta kwenye Kituo cha Usaidizi
true
true
true
true
true
59
false
false