Sera za uchumaji wa mapato katika Video Fupi za YouTube

Ugavi wa mapato katika Video Fupi za YouTube ulianza tarehe 1 Februari, 2023. Pata maelezo zaidi kuhusu mabadiliko mapya katika masharti ya Mpango wa Washirika wa YouTube.

Washirika wanaochuma mapato wanaweza kupata pesa kupitia matangazo yanayotazamwa kati ya video moja na nyingine katika Mipasho ya Video Fupi. Muundo huu mpya wa ugavi wa mapato umechukua nafasi ya Hazina ya Video Fupi za YouTube.

Sera zinazotumika kwenye uchumaji wa mapato katika Video Fupi za YouTube

Iwapo unachuma mapato kwenye YouTube, ni muhimu chaneli yako ifuate Sera za uchumaji mapato kwenye chaneli za YouTube, ikiwa ni pamoja na sera zetu kuhusu maudhui yanayojirudia na yanayotumiwa tena. Hii pia inajumuisha Mwongozo wa Jumuiya, Sheria na Masharti, Hakimiliki na sera za mpango wa AdSense kwenye YouTube.

Kuwasha kipengele cha ugavi wa mapato ya matangazo ya Video Fupi

Ili kuanza kushiriki katika mapato ya utangazaji katika Video Fupi, washirika wanaochuma mapato watahitaji kukubali Sehemu ya Uchumaji Mapato katika Video Fupi, masharti yanayokuruhusu kuchuma mapato kupitia matangazo na YouTube Premium katika Mipasho ya Video Fupi. Ugavi wa mapato ya matangazo katika Video Fupi utatumika kwa utazamaji wa Video Fupi unaotimiza masharti kwenye chaneli yako kuanzia tarehe utakapokubali. Utazamaji wa Video Fupi uliojumlishwa kabla ya kukubali Sehemu ya Uchumaji Mapato katika Video Fupi hautimizi masharti ya ugavi wa mapato ya matangazo katika Video Fupi.

Maudhui yanayofaa kwa matangazo

Maudhui yote yanayotumika kuchuma mapato kupitia matangazo lazima yafuate mwongozo wetu wa maudhui yanayofaa watangazaji. Katika Video Fupi, utazamaji wa maudhui yanayofuata mwongozo wetu wa maudhui yanayofaa watangazaji ndio tu unafaa katika ugavi wa mapato.

Utazamaji wa Video Fupi ambao hautimizi masharti

Kwa madhumuni ya kukokotoa malipo, YouTube haitahesabu utazamaji wa Video Fupi katika hali ambazo utazamaji hautimizi masharti. Mifano ya hali ambapo Utazamaji wa Video Fupi usiotimiza masharti unaweza kutokea: 

  • Video Fupi zisizo halisi, kama vile klipu ambazo hazijahaririwa kutoka kwenye filamu au vipindi vya televisheni vya watu wengine, kupakia upya maudhui ya watayarishi wengine walioko YouTube au kwenye mfumo mwingine, au mikusanyiko ambapo maudhui halisi hayajawekwa
  • Utazamaji wa kughushi au usio halisi wa Video Fupi, kama vile kutoka kwa mibofyo ya kiotomatiki au vijibu vya kusogeza
  • Utazamaji wa Video Fupi ambazo hazifuati mwongozo wetu wa maudhui yanayofaa watangazaji

Miundo ya matangazo inayotimiza masharti ya ugavi wa mapato katika Video Fupi

MPYA: Mapato ya Utangazaji kwenye Video Fupi, Njia Mpya za Kujiunga na Mpango wa Washirika wa YouTube na Shukrani Moto kwenye Video Fupi!

Mapato hugawanywa miongoni mwa matangazo ambayo yanatazamwa katikati ya video katika Mipasho ya Video Fupi. Ugavi wa mapato ya matangazo katika utazamaji wa Video Fupi unatokana tu na Mipasho ya Video Fupi, hali ambayo ni tofauti na uchumaji wa mapato wa video ndefu kwenye Ukurasa wa Kutazama.

Utaratibu wa ugavi wa mapato ya matangazo katika Video Fupi

MPYA: Ugavi wa Mapato ya Matangazo kwenye Video Fupi

Washirika wanaochuma mapato ambao wamekubali Sehemu ya Uchumaji Mapato katika Video Fupi ndio tu wanaweza kuchuma mapato ya matangazo kupitia Video Fupi.

Kuna hatua nne za jinsi ugavi wa mapato ya matangazo katika Video Fupi unavyofanya kazi:

  1. Ujumlishaji wa mapato ya matangazo kutoka Mipasho ya Video Fupi. Kila mwezi, mapato kutokana na matangazo yanayoonyeshwa katikati ya video katika Mipasho ya Video Fupi hujumlishwa na kutumiwa kuwalipa watayarishi na kusaidia kulipa gharama za leseni za muziki. 
     
  2. Kukokotoa Jumla ya Mapato ya Watayarishi yanayotokana na Video Fupi. Kisha, mapato ya matangazo kutoka Mipasho ya Video Fupi huwekwa kwenye Jumla ya Mapato ya Watayarishi yanayotokana na Video Fupi kulingana na utazamaji pamoja na matumizi ya muziki kwenye Video Fupi zilizopakiwa na watayarishi wanaochuma mapato. 
    • Ikiwa mtayarishi anayechuma mapato amepakia Video Fupi bila muziki wowote, mapato yote yanayohusishwa na utazamaji wake yataelekezwa kwenye Jumla ya Mapato ya Watayarishi yanayotokana na Video Fupi.
    • Iwapo mtayarishi anayetimiza masharti amepakia Video Fupi iliyo na muziki, basi YouTube itagawanya mapato yanayohusiana na utazamaji wake kati ya Jumla ya Mapato ya Watayarishi yanayotokana na Video Fupi na washirika wa muziki kulingana na idadi ya nyimbo zilizotumiwa.
Kwa mfano, iwapo mtayarishi anayechuma mapato atapakia Video Fupi iliyo na wimbo 1, nusu ya mapato yanayohusishwa na utazamaji wake yatawekwa kwenye Jumla ya Mapato ya Watayarishi yanayotokana na Video Fupi na nusu nyingine itatumiwa kulipia gharama za leseni za muziki. Iwapo Video Fupi ina nyimbo 2 za muziki, basi theluthi moja ya mapato yanayohusishwa na utazamaji wake yatawekwa kwenye Jumla ya Mapato ya Watayarishi yanayotokana na Video Fupi, na theluthi mbili nyingine zitatumiwa kulipia gharama za leseni za muziki. 
  1. Kuweka kwenye Jumla ya Mapato ya Watayarishi yanayotokana na Video Fupi. Kutoka katika kiasi cha jumla kwenye Jumla ya Mapato ya Watayarishi yanayotokana na Video Fupi, mapato yanasambazwa kwa watayarishi wanaochuma mapato kulingana na mgawo wao wa jumla ya utazamaji kutoka kwenye Video Fupi za mtayarishi anayechuma mapato katika kila nchi. Kwa mfano, iwapo mtayarishi atapata asilimia 5 ya utazamaji wote unaotimiza masharti wa Video Fupi iliyopakiwa na watayarishi wanaochuma mapato, atapewa asilimia 5 ya mapato katika Jumla ya Mapato ya Watayarishi yanayotokana na Video Fupi.
     
  2. Kutekeleza ugavi wa mapato. Watayarishi wanaochuma mapato watapokea asilimia 45 ya mapato yaliyotolewa, bila kuzingatia iwapo muziki ulitumiwa au haukutumiwa.

Yasiyojumuishwa katika Jumla ya Mapato ya Watayarishi yanayotokana na Video Fupi:

  • Mapato yanayohusiana na utazamaji wa Video Fupi zilizopakiwa na watayarishi ambao bado hawajakubali Sehemu ya Uchumaji Mapato katika Video Fupi, au bado hawajatimiza masharti ya kuchuma mapato kwenye Video zao Fupi. Mapato haya yatatumiwa kugharimia leseni za muziki na/au yatahifadhiwa na YouTube. 
  • Mapato yanayohusishwa na utazamaji wa Video Fupi zilizopakiwa na washirika wa muziki.
  • Mapato yanayohusiana na utazamaji wa Video Fupi ambazo zimebainishwa kuwa hazitimizi masharti.
  • Mapato yanayohusiana na matangazo yoyote yanayoonyeshwa baada ya kufungua Mipasho ya Video Fupi kabla ya kutazama Video Fupi (k.m. Bango Kuu la Video Fupi za YouTube).
  • Mapato yanayohusiana na matangazo yoyote yanayoonyeshwa kwenye kurasa za usogezaji ndani ya kichezaji cha Video Fupi.

Fahamu kupitia mfano

Tukague mfano wa kinadharia ili kufahamu vyema kuhusu utaratibu wake.

Mfano wa kinadharia

Ukiwa mtayarishi anayechuma mapato, tuchukulie kuwa umepakia Video Fupi ambayo inatumia wimbo 1 wa muziki. Hivi ndivyo tungekokotoa mapato yako ya Video Fupi katika Nchi A mwezi huu.

  • Video Fupi zimetazamwa kwa jumla ya mara milioni 100 katika Nchi A na utazamaji wote ni wa Video Fupi zilizopakiwa na watayarishi wanaochuma mapato.
  • $100,000 zimechumwa kupitia matangazo yanayoonyeshwa katikati ya Video Fupi katika Mipasho ya Video Fupi.
  • Asilimia 20 ya Video hizi Fupi zimetumia wimbo 1 wa muziki, kwa hivyo Jumla ya Mapato ya Watayarishi yanayotokana na Video Fupi ni $90,000 na $10,000 zitatumiwa kulipia gharama za leseni za muziki.
  • Video yako Fupi imetazamwa mara milioni 1, kwa hivyo utapewa asilimia 1 ya Jumla ya Mapato ya Watayarishi yanayotokana na Video Fupi, au $900. Mgawo wako kutoka kwenye Jumla ya Mapato ya Watayarishi yanayotokana na Video Fupi hauathiriwi na matumizi yako ya muziki.
  • Kisha, asilimia 45 ya ugavi wa mapato itatumika kwenye mgawo wako, na utapata $405 kutokana na utazamaji wa Video zako Fupi katika Nchi A.

Kutumia maudhui ya wengine katika Video Fupi

Katika hali fulani, wakati Video Fupi inaangazia maudhui ya wengine au maudhui mseto, utazamaji wa Video Fupi utagawanywa kati ya aliyepakia na washirika wengine wowote wenye haki (wamiliki wa maudhui mengine yaliyotumiwa katika Video Fupi) kwa madhumuni ya kukokotoa Jumla ya Mapato ya Watayarishi yanayotokana na Video Fupi na ugavi wa mapato kwa watayarishi wanaochuma mapato. Sera zifuatazo zinafafanua jinsi hatua hii itakavyotekelezwa. Tunaweza kusasisha sera hizi na tutakuarifu kuhusu mabadiliko yoyote.

  • Jinsi utumiaji wa maudhui ya wengine unavyoathiri Jumla ya Mapato ya Watayarishi yanayotokana na Video Fupi. Jumla ya Mapato ya Watayarishi yanayotokana na Video Fupi inapokokotolewa, maudhui ya muziki yanayowekwa na washirika wa tasnia ya muziki kwenye YouTube au yanayozalishwa kupitia Dream Track yatahesabiwa kuwa yana mchango kwenye Video fupi. Hii inamaanisha kuwa maudhui ya muziki yanapotumiwa katika Video fupi tu ndiyo yatapunguza idadi ya utazamaji na mapato husika yanayowekwa kwenye Jumla ya Mapato ya Watayarishi yanayotokana na Video Fupi. Hakuna aina nyingine za maudhui ya wengine zitakazohesabiwa kuwa zina mchango katika Video Fupi wakati huu, hata kama sera ya uchumaji mapato ya Content ID imewekwa kwenye maudhui hayo. Hata hivyo, tuko katika hatua za mwanzo za kuandaa mfumo wetu wa uchumaji wa mapato kwa aina nyingine za maudhui. 
    • Mifano iliyo hapo juu inaonyesha jinsi utazamaji na mapato husika hugawanywa ili kukokotoa Jumla ya Mapato ya Watayarishi yanayotokana na Video Fupi pale maudhui ya muziki yanapotumika katika Video fupi.
  • Jinsi utumiaji wa maudhui ya wengine unavyoathiri ugavi wa mapato kutoka kwenye Jumla ya Mapato ya Watayarishi yanayotokana na Video Fupi. Watayarishi wanaochuma mapato wanapolipwa mgawo wao kutoka kwenye Jumla ya Mapato ya Watayarishi yanayotokana na Video Fupi, kila mtayarishi anayechuma mapato atapewa asilimia 100 ya jumla ya utazamaji kwenye Video Fupi bila kuzingatia iwapo muziki wowote umetumika kwenye Video Fupi (ikijumuisha muziki uliozalishwa kupitia Dream Track). Kwa hivyo, kutumia muziki katika Video Fupi hakutaathiri mgawo wa mtayarishi kwenye Jumla ya Mapato ya Watayarishi yanayotokana na Video Fupi au kiwango chake cha ugavi wa mapato.

Ugavi wa mapato ya Video Fupi katika usajili kwenye YouTube Premium

YouTube Premium ni chaguo la usajili unaolipishwa ambalo huwawezesha watumiaji wafurahie maudhui bila matangazo, uchezaji wa chinichini, kupakua video na uwezo maalum wa kufikia programu ya YouTube Music. Manufaa haya pia yanatumika kwenye utazamaji wa Video Fupi. 

YouTube italipa asilimia 45 ya mapato halisi kutoka YouTube Premium ambayo yanagawanywa kwa watayarishi wanaochuma mapato ya Video Fupi. Sehemu ya mapato ya YouTube Premium hugawanywa ili kulipia gharama za leseni za muziki. Malipo kwa kila mtayarishi yanatokana na mgawo wake wa utazamaji wa Video Fupi katika kila nchi.

Sehemu ya kuona mapato yako ya matangazo ya Mipasho ya Video Fupi

Takwimu za YouTube zitaanza kuonyesha makadirio ya kila siku ya mapato ya matangazo ya Mipasho ya Video Fupi pamoja na vipimo vingine vya utendaji vinapopatikana au kuanzia tarehe ambayo utaanza kuchuma mapato ya matangazo kwenye Video Fupi. Pata maelezo zaidi kuhusu jinsi ya kuangalia mapato yako ya YouTube.

Ratiba ya muda ya kima cha malipo na maelezo mengine ya AdSense katika YouTube yaliyopo yatatumika – pata maelezo zaidi kuhusu AdSense katika YouTube.

Kidhibiti Maudhui cha Studio

Kwa watumiaji wa Kidhibiti Maudhui cha Studio, ripoti zinazoweza kupakuliwa zitapatikana kufikia katikati ya mwezi Machi 2023 kwa washirika wasio wa muziki pekee. Ripoti hizi zitajumuisha maelezo ya mapato yaliyogawanywa kulingana na tarehe na nchi au eneo kwa Video zozote Fupi zinazotumika kuchuma mapato ambazo zimepakiwa na washirika husika.

Ungependa kupata maelezo zaidi kuhusu utendaji wa Video zako Fupi? Angalia Vidokezo vya Watayarishi katika Takwimu za YouTube!

Pata maelezo zaidi kuhusu uchumaji wa mapato katika Video Fupi za YouTube 

Kwa nini mapato ya matangazo katika Video Fupi yanajumlishwa?

Video Fupi hutumia muundo wa matangazo ambao ni tofauti na video ndefu, hali inayotuhitaji tutumie mbinu ya kipekee ya ugavi wa mapato. Kwa kujumlisha mapato kisha kuyasambaza kulingana na mgawo wa utazamaji, tunalenga kuwalipa watayarishi wote ambao wanachuma mapato kupitia Video Fupi, si tu wale wanaoweka tangazo karibu na video yao. Kama manufaa ya ziada, muundo huu pia unaondoa changamoto za leseni za muziki, hali inayowawezesha watayarishi kutimiza malengo yao ya ubunifu bila kuhofia kupokea mapato machache kutokana na utumiaji wa muziki.

Je, kiuhalisia watayarishi hupata asilimia 45 ya mapato ya Video Fupi?

Kila mwezi, mapato kutokana na matangazo yanayoonekana katikati ya video kwenye Mipasho ya Video Fupi hujumlishwa na kutumiwa kuwalipa watayarishi wa Video Fupi na kulipia gharama za leseni za muziki. Kutokana na kiasi cha jumla kinachogawanywa kwa watayarishi (pia hujulikana kama Jumla ya Mapato ya Watayarishi yanayotokana na Video Fupi), watayarishi hupokea asilimia 45 ya mapato, bila kuzingatia iwapo wanatumia muziki katika Video zao Fupi.

Unamaanisha nini hasa unaposema "muziki"?

"Muziki" katika muktadha wa Video Fupi hurejelea maudhui ambayo yanatolewa au kudaiwa na washirika wa tasnia ya muziki kwenye YouTube. Hii inaweza kujumuisha nyimbo au sauti halisi za muziki, video za muziki au maudhui mengine ya muziki kama vile mahojiano na wasanii. Pia inajumuisha maudhui ya muziki yanayozalishwa kupitia Dream Track.

Je, bado ninaweza kuchuma mapato kupitia Hazina ya Video Fupi?
Hapana, tangu kuzinduliwa kwa ugavi wa mapato ya matangazo katika Video Fupi tarehe 1 Februari 2023, watayarishi hawatachuma tena mapato kupitia Hazina ya Video Fupi. Tunatarajia kuwa wapokeaji wengi wa Hazina ya Video Fupi watachuma mapato zaidi kutokana na muundo huu mpya wa ugavi wa mapato na utatumika badala ya Hazina ya Video Fupi. Mialiko ya mwisho ya Hazina ya Video Fupi ya shughuli za Januari itatumwa katikati mwa Februari 2023 na malipo yatafanyika Machi (kwa kutegemea vima vya malipo na masharti yetu).

Video zangu Fupi zipo katika Mipasho ya Video Fupi, lakini sichumi mapato. Je, ninaweza kupata pesa kutokana na matangazo hayo bila kujiunga kwenye Mpango wa Washirika wa YouTube?

Hapana. Washirika wanaochuma mapato ambao wamekubali Sehemu ya Uchumaji Mapato katika Video Fupi ndio tu wanaoweza kuchuma mapato ya matangazo na YouTube Premium kupitia Video Fupi. Mapato yatakayosalia yatatumiwa kulipia gharama za leseni za muziki au yatahifadhiwa na YouTube.
Nitajuaje iwapo Video zangu Fupi zinatumika kuchuma mapato ya matangazo? Je, nifanyeje iwapo ningependa kusitisha uchumaji wa mapato ya matangazo kupitia Video Fupi?

Kuanzia tarehe utakapokubali Sehemu ya Uchumaji Mapato katika Video Fupi, utazamaji wa Video yoyote Fupi kwenye chaneli yako utazingatiwa kwenye ugavi wa mapato ya matangazo katika Video Fupi. Utazamaji wa Video Fupi zitakazopakiwa baada ya tarehe 1 Februari, 2023 pia utazingatiwa kiotomatiki kwenye ugavi wa mapato ya matangazo katika Video Fupi, hutahitaji tena kuwasha kipengele cha uchumaji wa mapato kwenye Video Fupi wakati wa kupakia, kama unavyofanya kwenye video ndefu. Utazamaji wa Video Fupi uliojumlishwa kabla ya kukubali Sehemu ya Uchumaji Mapato katika Video Fupi hautimizi masharti ya ugavi wa mapato ya matangazo katika Video Fupi.

Baada ya kupakia Video yako Fupi, unaweza kuona hali yake ya uchumaji wa mapato katika sehemu ya Maudhui ya Studio ya YouTube. Video Fupi zenye utazamaji unaozingatiwa kwenye ugavi wa mapato ya matangazo katika Video Fupi zitaonyesha aikoni ya uchumaji wa mapato ya kijani au ya manjano. Pata maelezo zaidi kuhusu aikoni tofauti katika Mwongozo wetu wa aikoni za uchumaji wa mapato.

Takwimu za YouTube zitaanza pia kuonyesha makadirio ya kila siku ya mapato ya matangazo kutoka Mipasho ya Video Fupi pamoja na vipimo vingine vya utendaji, tarehe ambayo utaanza kuchuma mapato ya matangazo kwenye Video Fupi. Pata maelezo zaidi kuhusu jinsi ya kuangalia mapato yako ya YouTube.

Iwapo hungependa tena kuchuma mapato kupitia matangazo katika utazamaji wa Video Fupi kwenye chaneli yako, unaweza kujiondoa kwenye Sehemu ya Uchumaji Mapato katika Video Fupi kwa kuwasiliana na Usaidizi kwa Watayarishi.

Je, maelezo haya yamekufaa?

Tunawezaje kuboresha?
Tafuta
Futa utafutaji
Funga kisanduku cha kutafutia
Menyu kuu
15186153650342778962
true
Tafuta kwenye Kituo cha Usaidizi
true
true
true
true
true
59
false
false