Namna usajili unavyotumika

Mnamo mwezi Mei 2022, tulifanya mabadiliko katika namna ambayo bidhaa zinazolipiwa zinabainishwa na kudhibitiwa kwenye Dashibodi ya Google Play. Iwapo una usajili uliopo na unahitaji kufahamu jinsi mabadiliko haya yatakavyoathiri usajili wako, soma Mabadiliko ya usajili ya hivi majuzi kwenye Dashibodi ya Google Play.

Kwa kutumia Mfumo wa utozaji wa Google Play,  unaweza kuweka bidhaa za ndani ya programu zinazowatoza watumiaji kutumia maudhui au huduma katika vipindi vinavyojirudia, vinavyojulikana kama usajili. Usajili unaweza kujumuisha vipengele kama vile mkusanyiko wa programu, michezo au maudhui mengine ambayo hutoza ada inayojirudia katika programu yako kwenye Google Play.

Mfumo wa usajili wa Google Play unakupatia urahisi katika namna unavyoanzisha, kusimamia na kuuza usajili. Kwa kutumia Dashibodi ya Google Play au API ya Kuchapisha Usajili, unaweza kuweka mipangilio ya usajili mmoja wenye mipango ya msingi kadhaa, kila mmoja ukiwa na ofa kadhaa. Ofa za usajili zinaweza kuwa na miundo mbalimbali ya bei na chaguo za vigezo vya kujiunga. Unaweza kuweka ofa katika kipindi chote cha usajili, ukitumia aina mbalimbali za kusasisha kiotomatiki na mipango ya kulipia mapema.

Makala haya yanaelezea utendaji kazi wa usajili. Ili kuelewa namna ya kuanzisha na kusimamia usajili kwenye Dashibodi ya Google Play, nenda kwenye Anzisha na usimamie usajili. Ili kuelewa namna ya kutekeleza usajili kwenye Programu yako ya Android na sehemu ya nyuma ya mfumo wa kompyuta au programu, tembelea tovuti ya Wasanidi Programu wa Android.

Muhimu: Pamoja na maelezo yaliyo kwenye ukurasa huu, unapaswa urejelee Sera za Google Play za Mpango wa Wasanidi Programu, ikiwa ni pamoja na sera ya Usajili.

Muhtasari wa usajili

Sehemu hii inatambulisha dhana, vipengee na utendaji kazi wa usajili.

Vipengee vitatu vya usajili ni:

  • Usajili: Kipengee cha usajili kinabainisha seti ya manufaa ambayo watumiaji wanaweza kuyapata katika wakati uliobainishwa.
  • Mpango wa Msingi: Mpango wa msingi unabainisha kipindi cha bili ya usajili, aina ya usasishaji (kusasisha kiotomatiki au kulipia mapema) na bei. Usajili mmoja unaweza kuwa na mipango ya msingi kadhaa.
  • Ofa: Ofa inafafanua punguzo zinazopatikana kwa watumiaji waliokidhi vigezo. Mpango wa msingi mmoja unaweza kuwa na ofa kadhaa.

Picha iliyo hapa chini inaonyesha jinsi aina za vipengee vya usajili zinavyoundwa:

Usajili

Usajili ni seti ya manufaa ambayo watumiaji wanaweza kuyapata kwa kipindi cha muda kilichobainishwa. Unaweza kuwa na mipango mbalimbali ya usajili kwenye programu moja, inayoweza kuwakilisha manufaa tofauti kabisa (kwa mfano, programu ya kutiririsha video inaweza kuwa na usajili tofauti wa habari na michezo) au madaraja tofauti yenye manufaa ya aina moja (kwa mfano, programu ya hifadhi ya wingu inaweza kuwa na usajili wa GB 100, TB 1 na TB 10).

Watumiaji wanapata uwezo (au idhini) wa kufikia usajili kwa kulipia mpango wa msingi au ofa kwenye programu yako au kwenye Google Play.

Mpango wa msingi

Usajili huwa na mpango wa msingi mmoja au zaidi. Mpango wa msingi unabainisha jumla ya sifa za kipekee za kipindi husika cha malipo au aina ya usasishaji. Unaweza kubainisha iwapo usajili unasasishwa kiotomatiki (hujisasisha kiotomatiki) au hausasishwi kiotomatiki (kwa mpango wa kulipia mapema).

Usajili mmoja unaweza kuwa na mipango tofauti ya msingi. Kwa mfano, kwenye usajili mmoja wa "Uanachama wa Premium", unaweza kuanzisha mipango ya msingi ifuatayo:

  • Mpango wa msingi unaosasishwa kiotomatiki kila mwezi.
  • Mpango wa msingi wa kulipia mapema kila mwezi.
  • Mpango wa msingi unaosasishwa kiotomatiki kila mwaka.

Kumbuka: Kwa kila usajili, unaweza kuunda jumla ya pamoja ya hadi mipango ya msingi na ofa 250 na zisizozidi 50 zinazotumika kwa wakati mmoja. Zinazosalia ni lazima ziwe katika hali za rasimu au zisizotumika.

Kusasisha kiotomatiki

Watumiaji wanaweza kulipia mpango wa msingi unaosasishwa kiotomatiki ili kupata usajili kwa kipindi cha malipo kilichobainishwa, kinachotoza gharama za usajili kiotomatiki na kuongeza kipindi cha matumizi kila baada ya kipindi cha malipo kuisha. Mpango wa msingi unaosasishwa kiotomatiki humpa mtumiaji ruhusa ya kuwa na usajili usiokatizwa hadi pale atakapokatizwa. Usajili unaweza kukatizwa na mtumiaji, msanidi programu au mfumo wa utozaji wa Google Play.

Kulipia mapema

Watumiaji wanaweza kulipia mpango wa msingi wa kulipia mapema ili wapate usajili kwa kipindi cha bili kilichobainishwa ambacho hakisasishwi kiotomatiki. Watumiaji wanaweza kuongeza pesa baadaye ili wasogeze mbele muda wa tarehe ya mwisho ya mpango wa usajili na kuzuia kukatizwa kwa ufikiaji wa maudhui ya usajili.

Watumiaji wanapoongeza pesa, wanaweza kulipia mpango wowote wa msingi wa kulipia mapema unaopatikana kwenye usajili mahususi, ikijumuisha muda wa vipindi tofauti na vile walivyolipia hapo awali. Kwa mfano, mtumiaji mwenye mpango wa kulipia mapema wa mwezi mmoja wa $12.99 anaweza kuongeza pesa na kulipia $59.99 kupitia mpango wa kulipia mapema, inayowezesha kuongeza muda wa usajili kwa mwaka mmoja.

Pamoja na mfumo wa kuongeza pesa, watumiaji wanaweza pia kubadilisha kutoka katika mipango ya usajili ya kulipia mapema na kwenda mipango inayosasishwa kiotomatiki kadiri wanavyohitaji. Watumiaji wanaweza kufanya malipo haya kupitia programu yako au kituo cha usajili cha Duka la Google Play.

Malipo ya Awamu

Kumbuka: Kwa wakati huu, wasanidi programu wanaweza tu kutoa aina hii ya mpango wa msingi kwa watumiaji katika nchi zifuatazo: Brazili, Ufaransa, Italia na Uhispania.

Watumiaji wanaweza kununua mpango wa msingi wa unaolipiwa kwa awamu ili wapate usajili kwa kipindi cha malipo kilichobainishwa, kinacholipwa kwa awamu za kila mwezi. Waliojisajili ili walipe kwa awamu, hulipa kiasi kisichobadilika cha kila mwezi kwa muda wa kipindi cha usajili. Chaguo hili linaweza kutoa njia mbadala inayofaa kwa watumiaji ambao huenda wakapendelea kusambaza gharama ya usajili kadiri muda unavyosonga.

Wakati unaunda mpango wa msingi unaolipiwa kwa awamu, unatakiwa ubainishe kiasi cha malipo ya kila mwezi na kipindi cha malipo. Kwa mfano, ikiwa ungependa kutoa usajili wa miezi 12 katika programu yako ya mazoezi ambayo kwa kawaida huwa na bei ya $99.99, unaweza kutekeleza mpango wa msingi unaolipiwa kwa awamu kwa kiasi cha malipo ya kila mwezi cha $8.33 kwa kipindi cha malipo cha miezi 12.

Usajili wote unaolipiwa kwa awamu hulipwa katika vipindi vya kila mwezi; watumiaji na wasanidi programu hawawezi kurekebisha mara za kujirudia au muda wa malipo. Malipo ya wasanidi programu yatafanyika kadiri watumiaji wanavyofanya malipo yao ya kila mwezi. Wasanidi programu hawalipwi gharama za mapema mtumiaji anapojisajili.

Sifa za mpango wa msingi

Jedwali lifuatalo hapa chini linaorodhesha na kuelezea sehemu ambazo utazifafanua utakapoweka mipangilio yako ya mpango wa msingi kwenye Dashibodi ya Google Play:

Sehemu Maelezo
Kipindi cha malipo

Kipindi cha usajili.

Aina ya usasishaji

Iwe usajili unasasishwa kiotomatiki, unalipiwa mapema au unalipiwa kwa awamu (unapatikana kwa watumiaji katika nchi au maeneo mahususi).

Upatikanaji kulingana na eneo

Mpango wa msingi huwa na orodha ya mipangilio ya eneo ambayo inabainisha eneo ambalo mpango husika unapatikana pamoja na bei kwa kila eneo. Unaweza kudhibiti upatikanaji na mpangilio wa bei kwa kila nchi au eneo na uweke mipangilio iwapo unahitaji mpango wa msingi au ofa yako ipatikane kwenye maeneo mapya ambayo huduma za Google Play zitapatikana hapo baadaye.

Muda wa kutumia bila kutozwa Malipo ya usasishaji yakikataliwa, Google itamwomba mtumiaji arekebishe tatizo la malipo na ajaribu tena mara kwa mara kulipia usasishaji. Kwa chaguomsingi, kipindi hiki cha urejeshaji kinajumuisha muda wa kutumia bila kutozwa, kikifuatwa na kusimamisha akaunti kwa muda. Unaweza kubainisha urefu wa muda wa kutumia bila kutozwa, ambapo mtumiaji huhifadhi stahiki ya usajili.
Kusimamisha akaunti kwa muda Baada ya muda wowote wa kutumia bila kutozwa kukamilika bila tatizo la malipo kutatuliwa, usajili unaweza kuingia katika kipindi cha kusimamisha akaunti kwa muda. Unaweza kubainisha urefu wa kusimamisha akaunti kwa muda, wakati ambapo mtumiaji hapaswi kuwa na stahiki ya usajili. Iwapo kipindi cha kusimamisha akaunti kwa muda kitakamilika bila tatizo la malipo kutatuliwa, muda wa kutumia usajili utaisha kiotomatiki.
Mabadiliko ya mpango wa msingi na ofa

Iwapo mtumiaji ana usajili huu na amebadilisha kwenda kwenye mpango huu wa msingi au moja ya ofa za mpango huu wa msingi, hali kama hii ikitokea hubainishwa ni lini mtumiaji atozwe. Mpangilio huu hautumiki iwapo mtumiaji amebadilisha kwenda kwenye usajili mwingine.

Jisajili tena

Ikiwa imewashwa, watumiaji wanaweza kununua upya usajili wa kusasishwa kiotomatiki ambao muda wake umeisha kwenye Duka la Google Play.

Lebo

Lebo ni kitambulisho kisicho cha lazima chenye uwezo wa kuwekwa hadi herufi 20, unachoweza kutumia kuweka alama au kupanga makundi ya mipango ya msingi pamoja na ofa ili uzitambue kwenye API. Lebo zinaweza kutumika kubainisha ofa za kuonyesha kwa mtumiaji anapokidhi vigezo vya kupata ofa zaidi ya moja. Unaweza kuweka hadi lebo 20. Watumiaji hawawezi kuona lebo.

Ofa

Watumiaji wanaostahiki wanaweza kufurahia bei ya punguzo wanaponunua usajili. Ingawa mtumiaji yeyote anaweza kununua mpango wa msingi, ofa zinapatikana tu kwa watumiaji wanaokidhi masharti ya kujiunga uliyoyabainisha. Ofa zinaweza kumpatia mtumiaji majaribio yasiyolipishwa na/au bei ya utangulizi kupitia awamu za ofa moja au zaidi. 

Kwa kila usajili, unaweza kuunda jumla ya hadi mipango ya msingi na ofa 250 na zisizozidi 50 zinazotumika kwa wakati mmoja. Zinazosalia ni lazima ziwe katika hali ya rasimu au zisizotumika.

Madokezo:

  • Unaweza tu kutengeneza ofa kwa ajili ya mipango ya msingi ya kusasisha kiotomatiki.
  • Kwa kila usajili, unaweza kuunda jumla ya pamoja ya hadi mipango ya msingi na ofa 250 na zisizozidi 50 zinazotumika kwa wakati mmoja. Zinazosalia ni lazima ziwe katika hali ya rasimu au zisizotumika.

Masharti ya ofa

Unaweza kutoa ofa kwa watumiaji kulingana na hali zao za usajili kwenye programu yako. Unafanya hivi kwa kubainisha masharti ya kujiunga. Kuna hali tatu za matumizi zinazokubaliwa:

Hali ya matumizi Vigezo
Kupata mteja mpya

Mtumiaji hajawahi kuwa na haki ya usajili huu, au mteja hajawahi kuwa na haki ya usajili wowote kwenye programu hii.

Pata toleo jipya

Kwa sasa, mtumiaji ana usajili na kipindi mahususi cha bili kwenye programu hii. 

Kwa mfano, unaweza kubainisha ofa inayotoa bei ya utangulizi kwa usajili wa ngazi ya "Dhahabu" kwa watumiaji ambao wamesajiliwa katika ngazi ya "Fedha" kwa sasa.

Inabainishwa na msanidi programu

Unaamua mantiki ya biashara na kubainisha ustahiki kwenye programu yako. Mifano inajumuisha majaribio yasiyolipishwa ya mara ya pili au ofa za kuwasajili tena watumiaji ambao muda wao wa usajili umepita.

Kwa kuwa mantiki inakaa kwenye programu yako, ofa zilizobainishwa na msanidi programu haziwezi kuuzwa nje ya programu yako.

Awamu za ofa

Ofa zinajumuisha awamu moja au zaidi. Kila awamu inabainisha kipindi cha kutolipishwa au cha bei ya utangulizi. Kwa mfano, ofa inaweza kuwa na awamu ya jaribio lisilolipishwa la siku 7, ikafuatiwa na awamu ya utangulizi ya kulipia $2 kwa mwezi mmoja. Baada ya awamu za ofa ya punguzo kukamilika, usajili husasisha kiotomatiki ukitumia bei ya mpango msingi wa usajili.

Majaribio yasiyolipishwa

Awamu ya bei ya jaribio lisilolipishwa hutoa idadi mahususi ya siku, wiki au miezi bila malipo. Awamu za jaribio lisilolipishwa zinaweza kuwa kati ya siku 3 hadi miaka 3.

Kumbuka: Kwa mpango wa msingi unaolipiwa kwa awamu, awamu ya jaribio lisilolipishwa haihesabiki kama sehemu ya kipindi cha awali cha malipo.

Bei ya utangulizi

Awamu za bei ya utangulizi humpatia mtumiaji bei ya punguzo kwa muda usiobadilika. Awamu za bei ya utangulizi ni lazima ziwe sawa au pungufu ya bei ya mpango wa msingi. Zinaweza kuwa kamili au zinazofanana na bei ya mpango wa msingi. Bei zinazofanana zinaweza kurahisisha mabadiliko ya bei siku zijazo. Bei zinaweza kubainishwa kama ifuatavyo:

  • Kiasi kamili, kama vile $5
  • Punguzo lisilobadilika, kama vile punguzo la $5 la bei ya mpango wa msingi
  • Punguzo la asilimia, kama vile punguzo la asilimia 50 ya bei ya mpango wa msingi

Bei zote zinategemea bei ya kiwango cha chini na kiwango cha juu ya Google Play katika eneo ambapo bei husika inapatikana. Nenda kwenye Maeneo yanayoruhusiwa kwa ajili ya usambazaji kwa watumiaji wa Google Play ili kupata maelezo zaidi.

Kumbuka: Hali inayohusiana ya bei ya utangulizi kwa sasa haionyeshwi kwenye kikapu cha ununuzi. Kwa mfano, hakuna onyesho la mkato mlalo wa bei ya mpango wa msingi.

Awamu za bei ya utangulizi zinaweza kujumuisha aina moja au zaidi ya malipo:

  • Malipo ya mara moja: Awamu ya bei inayomtoza mtumiaji mara moja kwa idadi mahususi ya siku, wiki au miezi.
  • Malipo kadhaa: Awamu ya bei ambayo hutoa punguzo kati ya urudiaji wa mara 1 na 52 wa kipindi cha bili cha mpango wa msingi.

Kumbuka: Kwa mpango wa msingi unaolipiwa kwa awamu, awamu ya bei ya utangulizi huhesabiwa kama sehemu ya kipindi cha awali cha malipo. Kwa mfano, punguzo la matukio matatu yanayojirudia linaweza kuhesabiwa kama malipo matatu kati ya malipo ya kipindi cha awali cha malipo.

Sifa za ofa

Jedwali hapo chini linaorodhesha na kuelezea sehemu za ziada utakazozibainisha wakati unaweka ofa yako kwenye Dashibodi ya Google Play:

Sehemu Maelezo

Upatikanaji kulingana na eneo

Ofa hutumia hali chaguomsingi zinazopatikana kwenye eneo husika kuwa mpango wa msingi. Badala ya hivyo unaweza kuchagua sehemu ndogo ya maeneo hayo.

Lebo

Lebo ni kitambulisho kisicho cha lazima chenye uwezo wa kuwekwa hadi herufi 20, unachoweza kutumia kuweka alama au kupanga makundi ya mipango ya msingi pamoja na ofa ili uzitambue kwenye API. Lebo zinaweza kutumika kubainisha ofa za kuonyesha kwa mtumiaji anapokidhi vigezo vya kupata ofa zaidi ya moja. Ofa huonyesha lebo zake pamoja na lebo za mpango wa msingi unaohusiana nazo. Unaweza kuweka hadi lebo 20. Watumiaji hawawezi kuona lebo.

Kidokezo: Tunapendekeza utumie lebo kutambua ofa zilizowekwa zikiwa na ustahiki uliobainishwa na msanidi programu ili kusaidia kuzitofautisha wakati wa kuonyesha mkusanyiko wa ofa zinazopatikana kwa watumiaji.

Upatikanaji wa ofa na mpango wa msingi

Baada ya muda, unaweza kuweka na kurekebisha usajili, mipango ya msingi na ofa nyingi. Ingawa baadhi huenda hazitumiki tena, data ya kihistoria inaweza kuwa muhimu kwa madhumuni ya takwimu na ripoti. Vilevile, unaweza ukaweka njia mbadala za majaribio au kuhama kutoka kwenye ofa moja kwenda nyingine kulingana na misimu au sababu zingine. Mfumo mpya wa usajili hutumia hali hizi za utumiaji na hali za vipengee vya usajili. Ili kuhakikisha kuwa maelezo yanapatikana kila wakati kwa madhumuni ya kuripoti na uchanganuzi, huwezi kufuta usajili, mipango ya msingi na ofa au kutumia tena vitambulisho vyao.

Hali ya usajili

Vipengee vya usajili vinaweza kuwa na hali zifuatazo:

  • Rasimu: Usajili unaandaliwa na bado haujaanza kutumika. Usajili ukiwa katika hali ya rasimu, mipango yoyote ya msingi au ofa zilizowekwa pia huwa katika hali ya Rasimu.
  • Unatumika: Usajili upo na unaruhusu ununuzi uliopo. Iwapo kuna mipango yoyote ya msingi inayotumika, usajili pia huruhusu ununuzi mpya.
Hali ya mpango wa msingi na ofa

Ofa na mipango ya msingi inaweza kuwa na hali zifuatazo:

  • Rasimu: Mpango wa msingi au ofa inaandaliwa na bado haijaanza kutumika.
  • Hautumiki: Mpango wa msingi au ofa zipo, lakini haziruhusu ununuzi mpya. Usajili uliopo unaendelea hadi utakapoghairiwa. Unaweza kugeuza ofa kuwa inayotumika na isiyotumika kadiri inapohitajika.
  • Unatumika: Mpango wa msingi au ofa zipo na zinaruhusu ununuzi uliopo na mpya.

Hali ya matumizi ya kawaida ya mipango ya msingi na ofa

Sehemu hii inakupatia mifano ya mipangilio ya mipango ya msingi na ofa za kawaida. Bofya sehemu inayofuata hapo chini ili uone mfano.

Mpango wa kila mwezi unapatikana kwa mtumiaji yeyote

Mfano ufuatao unafafanua usajili wa msingi wenye mpango mmoja wa msingi wa kila mwezi kwa watumiaji wote katika maeneo mahususi. Hakuna ofa zozote wakati huu.

Maelezo ya usajili:

  • Jina: "Ufikiaji bila kikomo"
  • Manufaa ya mtumiaji:
    • "Ufikiaji bila kikomo kwenye vituo vyote"
    • "Bila matangazo

Maelezo ya mpango wa msingi:

  • Kipindi cha bili: Kila mwezi
  • Aina ya usasishaji:Usasishaji kiotomatiki
  • Upatikanaji kulingana na eneo:
    • Marekani 
    • Kanada
    • Uturuki
  • Bei kulingana na eneo:
    • Marekani: $9.99
    • Kanada: CA$10.99
    • Uturuki: TRY 155
  • Muda wa kutumia bila kutozwa: siku 7
Jaribio lisilolipishwa kwa watumiaji wapya

Ofa ifuatayo inatokana na mfano uliotangulia (Mpango wa kila mwezi unapatikana kwa mtumiaji yeyote), kuweka jaribio lisilolipishwa kwa watumiaji wapya kwa kubainisha ofa ifuatayo kwenye Dashibodi ya Google Play. Kumbuka kuwa ofa hii inatumika kwenye sehemu ndogo ya maeneo ya mpango wa msingi, haijumuishi Uturuki.

Ofa Maelezo:

  • Masharti ya kujiunga: Kupata mteja mpya
    • Hujawahi kuwa na usajili katika programu hii
  • Upatikanaji kulingana na eneo: (kumbuka kuwa Uturuki haijumuishwi)
    • Marekani
    • Kanada
  • Bei ya awamu ya 1:
    • Aina: Jaribio lisilolipishwa
    • Muda: Siku 7 (kisha inakuwa mpango wa msingi)

Hivi ndivyo inavyoweza kufanya kazi kwa mtumiaji:

  • Waliojisajili wapya (nchini Marekani na Kanada tu) watapata jaribio lisilolipishwa la siku 7.
  • Baada ya kipindi cha kujaribu kuisha, aliyejisajili atasasisha kiotomatiki na kupata bei ya kawaida ya mpango wa msingi.
  • Watumiaji wowote ambao hapo awali walinunua usajili wowote katika programu hii hawastahiki kupata ofa, hivyo wanaweza tu kununua mpango wa msingi.
Jaribio lisilolipishwa, likifuatiwa na bei ya utangulizi (kwa waliojisajili wapya)

Mfano ufuatao unatokana na mpango wa msingi katika mfano uliotangulia (Mpango wa kila mwezi unaopatikana kwa mtumiaji yeyote), kuweka ofa yenye awamu mbili za bei:

Ofa Maelezo:

  • Masharti ya kujiunga: Kupata mteja mpya
    • Hujawahi kuwa na usajili katika programu hii
  • Upatikanaji kulingana na eneo: (kumbuka kuwa Uturuki haijumuishwi)
    • Marekani
    • Kanada
  • Bei ya awamu ya 1:
    • Aina: Jaribio lisilolipishwa
    • Muda: Siku 7
  • Bei ya awamu ya 2:
    • Aina: Malipo ya wakati mmoja
    • Muda: Mwezi 1
    • Kubatilisha bei:  Kiasi kisichobadilika
    • Bei kulingana na eneo: 
      • Marekani: $1.99
      • Kanada CA$1.99

Hivi ndivyo inavyoweza kufanya kazi kwa mtumiaji:

  • Waliojisajili wapya (nchini Marekani na Kanada pekee) watapokea jaribio lisilolipishwa la siku 7, likifuatiwa na mwezi 1 wa kulipia $1.99/CA$1.99.
  • Baada ya kipindi cha kujaribu kuisha, aliyejisajili atasasisha kiotomatiki na kupata bei ya kawaida ya mpango wa msingi.
  • Watumiaji wowote ambao hapo awali walinunua usajili wowote katika programu hii hawastahiki kupata ofa, hivyo wanaweza tu kununua mpango wa msingi.
Ofa iliyobainishwa na msanidi programu, watumiaji wanaojisajili tena

Google Play hutoa usaidizi kwa hali za matumizi ya kawaida ya ustahiki, kama vile kupata mteja mpya. Programu yako pia inaweza kutathimini kulingana na masharti yako mwenyewe ya kujiunga, iwe ni pamoja na au badala ya ustahiki unaobainishwa na Google Play. Hali hii inamaanisha kwamba unaweza kuweka mantiki ya ziada pamoja na masharti ya kujiunga yaliyotathminiwa na Google Play na kuamua ofa unazotaka kuzipa kipaumbele na kuziwasilisha kwa watumiaji.  Kwa mfano, unaweza kuweka kikomo kwa waliojisajili wa awali ambao hapo awali walighairi kwa lengo la kuwauzia usajili tena.

Mfano ufuatao unatokana na mpango wa msingi katika mfano uliotangulia (Mpango wa kila mwezi unapatikana kwa mtumiaji yeyote), kuweka ofa iliyobainishwa na msanidi programu kwa kulipa nusu ya bei kwa miezi 3: 

Maelezo ya ofa:

  • Masharti ya kujiunga: 
    • Inabainishwa na msanidi programu 
  • Upatikanaji kulingana na eneo:
    • Marekani
    • Kanada 
  • Bei ya awamu ya 1:
    • Aina: Malipo yanayorudiwa
    • Vipindi vya bili: 3
    • Kubatilisha bei: Asilimia ya punguzo
    • Asilimia ya punguzo kulingana na eneo: 
      • Marekani: Asilimia 50
      • Kanada: Asilimia 50
  • Lebo:  PUNGUZO LA ASILIMIA 50 KWA WATUMIAJI WANAOJISAJILI TENA

Hivi ndivyo inavyoweza kufanya kazi kwa mtumiaji:

  • Watumiaji (nchini Marekani na Kanada pekee) wanaooneshwa ofa hii kwa kutumia mantiki ya ndani ya programu watapokea punguzo la asilimia 50 ya bei yao kwa miezi 3 (yaani, $4.99/CA$4.99).
  • Baada ya ofa kuisha, aliyejisajili atasasisha kiotomatiki na kupata bei ya kawaida ya mpango wa msingi.

Kumbuka: Ofa zozote zinazopatikana kwa ajili ya ununuzi wa nje ya programu, ikijumuisha usajili unaoangaziwa, haziwezi kuwa na vigezo vilivyobainishwa na msanidi programu.

Kidokezo: Tunapendekeza utumie lebo kutambua ofa zilizowekwa zikiwa na ustahiki uliobainishwa na msanidi programu ili kusaidia kuzitofautisha wakati wa kuonyesha mkusanyiko wa ofa zinazopatikana kwa watumiaji.

Jinsi ya kubadilisha mpango wa msingi na bei za ofa

Unaweza kubadilisha bei ya mpango wa msingi au ofa yoyote. Bei mpya inatumika papo hapo kwa ununuzi wowote mpya, ikijumuisha ununuzi wa kuongeza pesa wa mpango wa kulipia mapema.

Iwapo utabadilisha bei ya mpango wa msingi unaojisasisha kiotomatiki, watumiaji wowote waliokuwa wakilipa bei ya awali watawekwa katika kundi jipya la bei iliyopitwa na wakati. Watumiaji walio kwenye kundi la bei iliyopitwa na wakati wataendelea kulipa bei ya sasa hadi wabadilishe mpango wa usajili au hadi uamue kuwahamishia kwenye bei ya sasa. Kila wakati unapobadilisha bei, kundi jipya la bei iliyopitwa na wakati huundwa.

Kuhitimisha bei zilizopitwa na wakati

Unaweza kuamua kuhitimisha kundi la bei iliyopitwa na wakati na kuwahamishia watumiaji hao kwenye bei ya sasa ya mpango wa msingi. Hata hivyo, kumbuka yafuatayo:

  • Kuhitimisha kundi la bei iliyopitwa na wakati kunaweza tu kuathiri bei ya mpango wa msingi; haiwezekani kubadilisha bei ya awamu yoyote ya ofa baada ya ununuzi.
  • Pia, haiwezekani kuhamishia kundi la bei iliyopitwa na wakati kwenye bei yoyote, isipokuwa kwenye bei ya sasa ya mpango wa msingi.
  • Kuhitimisha kundi la bei iliyopitwa na wakati kutahitimisha pia makundi yoyote ya awali ya mpango huo huo wa msingi.

Kumbuka: Kwa mpango wa msingi unaolipiwa kwa awamu, iwapo msanidi programu angependa abadilishe bei (au ikiwa mtumiaji angependa akatishe), badiliko huanza kutumika mwishoni mwa kipindi cha malipo.

Punguzo la bei

Iwapo bei mpya ni ya kiwango cha chini, punguzo la bei linalotokana na bei hiyo linawekwa kiotomatiki na halihitaji kuidhinishwa na mtumiaji. Watumiaji wanapewa arifa na wanatozwa bei ya chini katika tarehe inayofuata ya usasishaji wao.

Ongezeko la bei

Iwapo bei mpya ni ya kiwango cha juu, ongezeko la bei linalotokana na bei hiyo litakuwa ni la kujijumuisha au kujiondoa.

Ongezeko la bei unalofaa kujijumuisha

Kwenye ongezeko la bei unalofaa kujijumuisha, ni lazima mtumiaji akubali ongezeko la bei kabla halijaanza kutumika. Mtumiaji asipokubali, usajili wake hukatishwa kiotomatiki kabla hajatozwa kwa mara ya kwanza bei iliyoongezwa. Watumiaji watakuwa na kipindi cha angalau siku 30 baada ya kupokea arifa ili kujijumuisha, hatua ambayo inaweza kusababisha kiwango cha tozo inayofuata kisalie katika bei ya sasa.

Kidokezo: Ongezeko la bei unalofaa kujijumuisha linaweza kusababisha ongezeko la watumiaji wanaojiondoa iwapo hawatakubali mabadiliko ya bei. Tunapendekeza uwasiliane na watumiaji walioathiriwa mapema ili uwakumbushe kuhusu manufaa wanayopata.

Ongezeko la bei unalofaa kujiondoa

Katika mazingira fulani, unaweza kuongeza bei kwa kutuma arifa ya mapema kwa watumiaji, lakini bila kuwahitaji kuchukua hatua yoyote ya ziada. Hali hii inajulikana kama ongezeko la bei unalofaa kujiondoa.

Watumiaji wanaweza kukatisha usajili wao wakipenda, vinginevyo watatozwa bei mpya kwenye usasishaji unaofuata baada ya kipindi cha arifa. Kipindi hiki ni angalau siku 30 au siku 60, kulingana na nchi au eneo. Kipindi cha arifa kinaweza kusababisha usasishaji zaidi kwa bei ya sasa.

Ongezeko la bei unalofaa kujiondoa ni lazima litimize vigezo vifuatavyo:

  • Ongezeko la bei unalofaa kujiondoa linapatikana katika maeneo au nchi fulani pekee na kwa wasanidi programu wenye hadhi nzuri kwenye Google Play. Ili upate maelezo zaidi, angalia maeneo au nchi linapotumika na vipindi vyao vya chini zaidi vya arifa ya mapema.

Ongezeko la bei unalofaa kujiondoa pia linadhibitiwa na kiasi na urudiaji. Vigezo hivi hutekelezwa kwenye Kiolesura cha Dashibodi:

  • Kila mpango wa msingi wa usajili unaweza kuwa na ongezeko moja tu la bei unalofaa kuijiondoa kwa kila nchi au eneo katika siku 365 zilizopita.
  • Kiasi cha juu zaidi cha ongezeko la bei katika nchi au maeneo yote kinapaswa kuwa zaidi ya:
    • Asilimia 50 ya bei ambayo mtumiaji analipa kwa sasa; au
    • Senti 17 za Marekani kwa siku (zikiwa zimegeuzwa kuwa sarafu ya nchi ulimo inavyohitajika)

Ni wajibu wako kuhakikisha kuwa ongezeko la bei unalofaa kujiondoa linatimiza vigezo vifuatavyo. Unapoanzisha kila ongezeko la bei unalofaa kujiondoa, ni lazima uthibitishe kwenye Dashibodi ya Google Play kwamba:

  • Ni lazima sheria na masharti ya progamu yako yahifadhi haki yako ya kuongeza bei ya usajili kufuatia arifa ya mapema na kutoa sababu wazi na halisi za ongezeko kama hilo.
  • Angalau siku 30 kabla ya ongezeko la bei kuanza kutumika, utamwonyesha kila mtumiaji atakayeathiriwa arifa dhahiri ya ndani ya programu inayojumuisha angalau: jina la usajili wa mtumiaji, bei ya sasa na bei mpya, tarehe ambapo bei mpya itaanza kutumika kiotomatiki na maelezo kuhusu jinsi ya kukatisha usajili.

    Muhimu: Ni lazima arifa hii ionyeshwe kwenye aina zote za vifaa ambapo programu inapatikana, ikiwa ni pamoja na vifaa vya mkononi, mifumo ya televisheni na vifaa vya kutiririsha. Vifaa vya saa pekee ndivyo visivyofuata kanuni hii, ambapo arifa inapendekezwa lakini si lazima.

Iwapo ongezeko la bei halitimizi vigezo vyote vilivyo hapo juu, huwezi kuweka ongezeko la bei unalofaa kujiondoa. Badala yake, unaweza kuweka ongezeko la bei unalofaa kujijumuisha kwa makundi husika au kuyaacha makundi haya kwenye bei ya sasa.

Ongezeko la bei linaloingiliana

Baada ya kuanzishwa, shughuli za uhamishaji haziwezi kusimamishwa. Hata hivyo, iwapo unahamisha kundi la bei iliyopitwa na wakati kwa kutumia ongezeko la bei, kisha uanzishe uhamishaji mwingine wa mtumiaji huyo huyo, uhamishaji wa kwanza utasimamishwa. Hali hii haitaathiri watumiaji ambao hawajashughulikia ongezeko la kwanza la bei (iwe kwa kukubali ongezeko la bei au kutokana na kumalizika kwa kipindi chao cha arifa ya kujiondoa kwenye ongezeko la bei). Kwa watumiaji hao, ongezeko jipya la bei ndilo tu litatumika.

Malipo yaliyokataliwa, muda wa kutumia bila kutozwa na kusimamisha akaunti kwa muda

Ikiwa malipo ya usasishaji yatakataliwa, Google itamwomba mtumiaji atatue tatizo la malipo na ajaribu mara kwa mara kulipia usasishaji. Kwa chaguomsingi, kipindi hiki cha urejeshaji hujumuisha muda wa kutumia bila kutozwa ikifuatwa na kipindi cha kusimamisha akaunti kwa muda. Unaweza kubainisha urefu wa muda wa kutumia bila kutozwa, ambapo mtumiaji huhifadhi stahiki ya usajili.

Ikiwa tatizo la malipo halijatatuliwa baada ya muda wowote wa kutumia bila kutozwa kuisha, usajili unaweza kuingia katika kipindi cha kusimamisha akaunti kwa muda. Unaweza kubainisha urefu wa kusimamisha akaunti kwa muda, wakati ambapo mtumiaji hapaswi kuwa na stahiki ya usajili. Iwapo kipindi cha kusimamisha akaunti kwa muda kitaisha bila tatizo la malipo kutatuliwa, muda wa kutumia usajili utaisha kiotomatiki.

Kwa chaguomsingi, hali ya kusimamisha akaunti kwa muda imewashwa kwenye mipango yote ya msingi inayosasishwa kiotomatiki. Unaweza kurekebisha urefu wa kipindi cha kusimamisha akaunti kwa muda au kukizima kwenye Dashibodi ya Google Play. Ni lazima kipindi cha kusimamisha akaunti kwa muda na muda wa kutumia bila kutozwa uwe jumla ya siku 30 au zaidi.

Huenda kubainisha vipindi vifupi kuliko thamani chaguomsingi kukapunguza idadi ya usajili unaorejeshwa kutokana na malipo kukataliwa.

Kuruhusu kipengele cha kusimamisha usajili

Unaweza kuzuia hali ya kupunguza matukio ya kuondoka kwenye programu kwa hiari kwa kuwaruhusu watumiaji kusimamisha usajili wao. Unaporuhusu kipengele hiki, watumiaji wanaweza kuchagua kusimamisha usajili wao kwa muda wa kipindi fulani kati ya wiki moja na miezi mitatu badala ya kughairi, kulingana na kipindi cha malipo yanayojirudia. Kinapowashwa, chaguo la kipengele cha kusimamisha usajili huonekana katika kituo cha usajili na kwenye mtiririko wa kughairi. Kumbuka kuwa usajili wa kila mwaka na majaribio yasiyolipishwa hayawezi kusimamishwa.

Ili uruhusu watumiaji kusimamisha usajili wao:

  1. Fungua Dashibodi ya Google Play kisha uende kwenye ukurasa wa Mipangilio ya uchumaji wa mapato (Chuma mapato > Mipangilio ya uchumaji wa mapato).
  2. Katika sehemu ya "Mipangilio ya usajili", badilisha hali kutoka "Simamisha" kuwa Imewashwa.
  3. Bofya Hifadhi mabadiliko.

Hali ya kusimamisha usajili huanza tu baada ya kipindi cha bili cha sasa kuisha. Wakati usajili umesimamishwa, mtumiaji hawezi kufikia usajili. Mwishoni mwa kipindi cha kusimamisha usajili, usajili utaendelea na Google hujaribu kusasisha usajili. Ikiwa imefanikiwa kusasisha, usajili huanza kutumika tena. 

Pata maelezo zaidi kuhusu kusimamisha usajili na masharti ya kutekeleza tukio la kusimamisha usajili kwenye tovuti ya Wasanidi Programu wa Android.

Masharti ya kughairi usajili

Ili utii mabadiliko yajayo ya Sera ya Usajili ya Google Play, programu yako inapaswa ijumuishe njia iliyo rahisi kutumia ya mtandaoni kwa ajili ya waliojisajili kughairi usajili. Katika mipangilio ya akaunti ya programu yako (au sehemu sawa na hiyo), unaweza kutimiza masharti haya kwa kujumuisha:

  • kiungo cha Kituo cha Usajili cha Google Play (ikiwa programu yako inatumia mfumo wa utozaji wa Google Play); na/au
  • ufikiaji wa moja kwa moja kwenye mchakato wako wa kughairi.

Masharti yamebainishwa kwa kina kwenye sehemu ya Kudhibiti na kughairi usajili katika sera ya Usajili.

Je, maelezo haya yamekufaa?

Tunawezaje kuboresha?

Je, unahitaji usaidizi mwingine?

Jaribu hatua zifuatazo:

true
Tafuta
Futa utafutaji
Funga kisanduku cha kutafutia
Menyu kuu
415956383308144946
true
Tafuta kwenye Kituo cha Usaidizi
true
true
true
true
true
92637
false
false