Matumizi ya haki ni kanuni ya kisheria inayosema kwamba matumizi ya maudhui yanayolindwa na hakimiliki yanaruhusiwa katika hali fulani bila ya kuwa na ruhusa kutoka kwa mwenye hakimiliki.
YouTube hupokea maombi mengi ya kuondoa video ambazo wenye hakimiliki hudai kuwa zinakiuka hakimiliki chini ya sheria ya hakimiliki. Wakati mwingine maombi haya hutumika kwenye video zinazostahiki hali zinazoruhusiwa kutofuata kanuni za hakimiliki au zinazoonekana kuwa mifano dhahiri ya matumizi ya haki.
Iwapo matumizi ya maudhui yanayolindwa na hakimiliki katika video yanatimiza masharti ya kuwa hali inayoruhusiwa kutofuata kanuni za hakimiliki, basi video hiyo huchukuliwa kuwa halali na isiyokiuka sheria. Ndiyo maana mara nyingi huwa tunawaomba wenye hakimiliki wafikirie iwapo hali zinazoruhusiwa kutofuata kanuni za hakimiliki zinatumika kabla ya kutuma ombi la kuondoa video kwa kukiuka hakimiliki kwenye YouTube. Ikiwa mwenye hakimiliki anaamini kuwa video haistahiki hali inayoruhusiwa kutofuata kanuni, basi lazima atupe maelezo ya kutosha akituelezea kwa nini.
Hali zinazoruhusiwa kutofuata kanuni za hakimiliki kote duniani
Ingawa sheria za kimataifa kuhusu hali zinazoruhusiwa kutofuata kanuni za hakimiliki mara nyingi hufanana, zinaweza kutofautiana. Nchi na maeneo mbalimbali yanaweza kuwa na sheria tofauti kuhusu ni wakati upi ni sawa kutumia maudhui yanayolindwa na hakimiliki bila ya kuwa na ruhusa ya mwenye hakimiliki.
Nchini Marekani, kazi za kutoa maoni, kukosoa, kutafiti, kufunza au kuripoti habari zinaweza kuchukuliwa kuwa matumizi ya haki. Katika Umoja wa Ulaya, hali chache zaidi zisizofuata kanuni zinatambuliwa na ni lazima matumizi yalingane na kategoria mahususi, kama vile kunukuu, kukosoa, kuhakiki, kuchekesha, kubeza na kuiga watu wengine. Nchi au maeneo mengine yana dhana inayoitwa matumizi yasiyo ya biashara yanayoweza kufanya kazi kwa njia tofauti.
Hatimaye, mahakama huamua kesi za matumizi ya haki kulingana na ukweli wa kila kesi mahususi. Huenda ungependa kupata ushauri wa kisheria kutoka kwa mtaalamu kabla ya kupakia video zinazotumia maudhui yanayolindwa kwa hakimiliki.
Vigezo vinne vya matumizi ya haki
Nchini Marekani, mahakimu huamua kinachozingatiwa kuwa matumizi ya haki. Hakimu atazingatia jinsi vigezo hivyo vinne vya matumizi ya haki vinavyotumika kwa kila kesi. Vigezo hivyo vinne vya matumizi ya haki ni:
1. Madhumuni na sifa ya matumizi, ikiwa ni pamoja na iwapo utumiaji huo ni wa kibiashara au ni kwa madhumuni ya elimu bila manufaa ya kifedha
2. Asili ya kazi iliyo na hakimiliki
3. Kiasi na umuhimu wa sehemu iliyotumiwa ikilinganishwa na kazi nzima ya maudhui yaliyo na hakimiliki
4. Athari ya matumizi kwenye soko tarajiwa au thamani ya kazi ya maudhui yaliyo na hakimiliki
Mifano ya matumizi ya haki
Donald Duck Meets Glenn Beck in Right Wing Radio Duck |
"Donald Duck Anakutana na Glenn Beck katika Right Wing Radio Duck"kutoka rebelliouspixels Mseto huu unajumuisha makala mafupi kutoka nyenzo za vyanzo mbalimbali. Miseto hii hubuni ujumbe mpya kuhusu swali la balagha la kufikirisha katika nyakati za ugumu wa kiuchumi. Kazi zinazobuni maana mpya kuhusu maudhui halisi zinaweza kuchukuliwa kama matumizi ya haki. |
Mpango wa ulinzi wa matumizi ya haki wa YouTube
Katika matukio ambayo ni nadra, tumewaomba watayarishi wa YouTube wajiunge kwenye mpango unaolinda baadhi ya mifano ya “matumizi ya haki” kwenye YouTube kutokana na maombi ya kuondoa video kwa kukiuka hakimiliki. Kupitia mpango huu, YouTube huwafidia watayarishi ambao video zao za matumizi ya haki zimepokea maombi ya kuondoa kwa kiasi cha hadi dola milioni 1 za Marekani kutokana na gharama za kisheria katika tukio ambako uondoaji unasababisha mashtaka ya ukiukaji wa hakimiliki.
Lengo la mpango huu ni kuhakikisha kuwa watayarishi hawa wana fursa ya kulinda kazi zao. Pia, unalenga kuboresha ulimwengu wa ubunifu kwa kuelimisha kuhusu umuhimu na vikomo vya matumizi ya haki. Kwa sababu ya kutofautiana kwa sheria zinazoongoza matumizi kama haya katika nchi au maeneo mbalimbali, kama ilivyoelezwa hapo juu, tunaweza tu kutoa mpango huu kwa watayarishi wanaoishi Marekani ambao wanakubali video zao zipatikane nchini Marekani pekee.
Mifano ya video zilizo katika mpango wa ulinzi wa matumizi ya haki wa YouTube
Video hizi za mfano zinawakilisha sampuli ndogo ya kiasi kikubwa cha maombi tunayopokea ya kuondoa video kwa kukiuka hakimiliki. Zinawakilisha pia video chache kati ya idadi kubwa ya video zinazoweza kuwa na matumizi ya haki zinazoweza kuondolewa.
Kila mwaka, YouTube inaweza kutoa ulinzi wa matumizi ya haki kwa video chache tu, zinazochaguliwa kulingana na vigezo vingi. Kwa ujumla, tunachagua video zinazoonyesha vizuri zaidi matumizi ya haki kulingana na vigezo vinne vya matumizi ya haki.
Video za matumizi ya haki zilizorejeshwa
Ingawa YouTube haiwezi kutoa utetezi wa kisheria kwa kila mtu, tunaendelea kuwa macho kuhusu maombi ya kuondoa video kwa kukiuka hakimiliki yanayoathiri watayarishi wote wa YouTube.
Huenda unafahamu baadhi ya matukio muhimu ambapo tumewaomba wenye hakimiliki wazingatie upya maombi ya kuondoa na warejeshe video za matumizi ya haki. Kwa mfano:
- Video hii ya Young Turks, ambayo inaonyesha klipu fupi kutoka kwenye tangazo ambalo limekashifiwa zaidi kama sehemu ya mazungumzo kuhusu ni kwa nini iliwakera watazamaji.
- Video hii ya Secular Talk, ambayo inamkashifu mwanasiasa kwa kuidhinisha matibabu ambayo hayajathibitishwa ya kisukari.
- Buffy vs Edward: Twilight Remixed -- [toleo halisi], video mseto ambayo inalinganisha njia ambazo wanawake wanadhihirishwa katika kazi mbili zinazohusiana na wanyonya damu zinazolenga vijana.
- "No Offense", video iliyopakiwa na Shirika la Kitaifa la Ndoa, ambayo inatumia klipu ya mtu mashuhuri kama mfano wa tabia ya kiburi.
Maelezo zaidi
Iwapo ungependa kupata maelezo zaidi kuhusu matumizi ya haki, kuna nyenzo nyingi zinazopatikana mtandaoni. Tovuti zifuatazo ni za madhumuni ya kielimu pekee na hazijaidhinishwa na YouTube:
- Tovuti ya Center for Media and Social Impact ya “Kanuni ya Desturi Bora katika Matumizi ya Haki ya Video Mtandaoni”
- Tovuti ya Digital Media Law Project ya ufafanuzi wa kina wa Vigezo hivi Vinne
- Tovuti ya Ofisi ya Hakimiliki Marekani, faharasa ya matumizi ya haki