Kufumbua matumizi ya maudhui sanisi au yaliyobadilishwa

Tunawahimiza watayarishi watumie kiubunifu na kwa kuwajibika zana za kuhariri au kuzalisha maudhui. Wakati huo huo, tunatambua kuwa watazamaji wanataka kufahamu ikiwa maudhui wanayotazama au kusikiliza ni halisi.

Ili kusaidia kuwafahamisha watazamaji kuhusu maudhui wanayotazama, tunawahitaji watayarishi wafumbue maudhui yaliyobadilishwa kwa kiasi kikubwa au kuzalishwa kwa njia ya usanisi yanapoonekana kuwa halisi.

Lazima watayarishi wafumbue maudhui:

 • Yanayomfanya mtu halisi aonekane kusema au kufanya kitu ambacho hakufanya
 • Yanayobadilisha video ya mahali au tukio halisi
 • Yanayozalisha tukio linaloonekana kuwa la kweli ambalo halikutokea

Maudhui haya yanaweza kujumuisha yale yaliyobadilishwa au kutayarishwa kikamilifu au kwa kiasi fulani kwa kutumia zana za kutayarisha au kuhariri sauti, video au picha.

Kufumbua kwa kutumia mipangilio ya ‘maudhui yaliyobadilishwa’ kwenye Studio ya YouTube

Ili kufumbua maudhui yaliyobadilishwa kwa kiasi kikubwa au kuzalishwa kwa njia ya usanisi, mipangilio ya ‘maudhui yaliyobadilishwa’ inapatikana kwa watayarishi wanaotumia Studio ya YouTube kwenye kompyuta. Tutasambaza mipangilio hii kwenye vifaa vingine na programu za YouTube katika siku zijazo.

Baada ya mtayarishi kuchagua sehemu hii na kupakia maudhui, lebo itaonekana kwenye maelezo yaliyopanuliwa ya video yake.

Watayarishi wanaotayarisha Video Fupi za YouTube kwa kutumia Dream Track au Dream Screen, zana za akiliunde (AI) zalishi za YouTube, hawapaswi kuchukua hatua za ziada ili kufumbua matumizi. Zana husika itafumbua kiotomatiki matumizi ya AI kwa watayarishi. Kwa zana nyingine za AI, watayarishi wanahitaji kufumbua matumizi yao wakati wa utaratibu wa kupakia.

Mifano ya maudhui sanisi au yaliyobadilishwa

Orodha ifuatayo inajumuisha mifano ya maudhui sanisi au yaliyobadilishwa. Maudhui sanisi au yaliyobadilishwa yanaweza kujumuisha yale yaliyobadilishwa au yaliyotayarishwa kikamilifu au kwa kiasi fulani kwa kutumia zana zozote za kutayarisha au kuhariri sauti, video au picha. Maudhui yanayofanana uhalisia na mabadiliko makubwa yanahitaji ufumbuzi, huku mabadiliko madogo au maudhui yasiyo halisi yakiwa hayahitaji kufumbuliwa. Kumbuka, hii si orodha kamili.

Hakuhitaji ufumbuzi wa watayarishi Kunahitaji ufumbuzi wa watayarishi
 • Kutumia madoido ya urembo
 • Kuzalisha au kubadilisha maudhui kidijitali ili kubadilisha uso wa mtu mmoja na kuweka wa mtu mwingine
 • Kuzalisha kwa njia ya usanisi au kupanua mandhari ili kuiga gari iliyo kwenye mwendo
 • Kubadilisha mandhari maarufu ya mbio za magari kidijitali ili kumjumuisha mtu mashuhuri ambaye hakuwa kwenye filamu halisi
 • Kutumia madoido ili kuboresha sauti iliyorekodiwa hapo awali
 • Kuiga sauti ili kuifanya isikike kana kwamba mtaalamu wa matibabu alitoa ushauri wakati mtaalamu hakutoa ushauri huo
 • Kutumia uhuishaji wa kombora uliotayarishwa kwa AI kwenye video
 • Kuonyesha taswira inayofanana uhalisia wa kombora likirushwa kwenye jiji halisi

 

Mifano ya maudhui ambayo si lazima watayarishi wayafumbue
Watayarishi hawahitaji kufumbua maelezo kuhusu maudhui yasiyo ya kweli ambayo ni sanisi au yaliyobadilishwa au mabadiliko madogo kwenye maudhui halisi. Mabadiliko madogo ni yale ambayo kimsingi ni ya usanifu na hayabadilishi maudhui katika namna ambayo yanaweza kumpotosha mtazamaji kuhusu kilichotokea.
Mifano ya maudhui, mabadiliko au usaidizi wa kutayarisha video ambao watayarishi hawapaswi kufumbua:
 • Yasiyo halisi
  • Mtu anayeendesha mnyama kama farasi mwenye pembe moja katika ulimwengu wa kustaajabisha
  • Skrini ya kijani inapotumika kuonyesha mtu akielea angani
 • Mabadiliko madogo
  • Marekebisho ya rangi au madoido ya mwangaza
  • Madoido maalum, kama vile kuweka madoido ya ukale au kutia ukungu mandharinyuma
  • Usaidizi wa utayarishaji maudhui, kama vile kutumia zana za AI zalishi kutayarisha au kuboresha hati, kijipicha, kichwa, mchoro wenye maelezo au muhtasari wa video
  • Utayarishaji wa manukuu
  • Kuongeza udhahiri, kuongeza ubora au kurekebisha video na kurekebisha sauti
  • Uibuaji wa mawazo

Kumbuka, orodha iliyo hapo juu si kamili.

Mifano ya maudhui ambayo watayarishi wanapaswa kufumbua maelezo kuyahusu
Ili kusaidia kuwafahamisha watazamaji kuhusu maudhui wanayotazama, tunawahitaji watayarishi wafumbue maudhui sanisi au yaliyobadilishwa yanapoonekana kuwa halisi au kufanyiwa mabadiliko kwa kiasi kikubwa.
Mifano ya maudhui, mabadiliko au usaidizi wa kutayarisha video ambao watayarishi wanapaswa kufumbua:
 • Kuzalisha muziki kwa njia ya usanisi (ikijumuisha muziki uliotayarishiwa kwa kutumia kipengele cha Muziki wa Watayarishi)
 • Kurudufisha sauti ya mtu mwingine ili kuitumia katika masimulizi
 • Kuzalisha video ya ziada ya eneo halisi kwa njia ya usanisi, kama vile video ya mtu anayeteleza kwenye mawimbi kisiwani Maui ili itumike katika video ya utangazaji wa safari
 • Kuzalisha video inayofanana uhalisia inayoonyesha mechi kati ya wachezaji wawili wa kulipwa wa tenisi kwa njia ya usanisi
 • Kufanya ionekane kana kwamba mtu alitoa ushauri ambao hakuutoa
 • Kubadilisha sauti kidijitali ili kuifanya ionekane kana kwamba mwimbaji maarufu alikosea noti ya muziki wakati wa tamasha lake mubashara
 • Kuonyesha taswira inayofanana uhalisia wa kimbunga au matukio mengine ya hali ya hewa yanayoelekea kwenye jiji halisi ambayo hayakutokea
 • Kufanya ionekane kana kwamba wafanyakazi wa hospitali wamekataa kuwahudumia wagonjwa au majeruhi
 • Kumfanya mtu maarufu aonekane akiiba kitu ambacho hakuiba au akikubali kuiba kitu wakati hakukubali
 • Kufanya ionekane kama mtu halisi amekamatwa au amefungwa

Kumbuka, orodha iliyo hapo juu si kamili.

Kufumbua maudhui sanisi au yaliyobadilishwa

Tunahitaji watayarishi wafumbue maudhui yaliyobadilishwa kwa kiasi kikubwa au yaliyozalishwa kwa njia ya usanisi yanayoonekana kuwa halisi. Watayarishi wanaweza kufanya ufumbuzi huu wakati wa kupakia maudhui.

Studio ya YouTube kwenye kompyuta

 1. Nenda kwenye Studio ya YouTube.
 2. Fuata hatua za kupakia maudhui.
 3. Katika sehemu ya Maelezo, chini ya “Maudhui yaliyobadilishwa,” chagua Ndiyo ili ujibu maswali yote ya ufumbuzi.
 4. Endelea ili uchague maelezo mengine ya video.

Ikiwa mtayarishi atatayarisha Video Fupi ya YouTube inayotumia mojawapo ya madoido ya akiliunde (AI) zalishi ya YouTube (kama vile Dream Track au Dream Screen ya YouTube), hakuna hatua za ziada zinazohitajika ili kufumbua kwa sasa. Zana husika itafumbua kiotomatiki matumizi ya AI kwa watayarishi.

Ili kuwasaidia watayarishi, huenda tukachagua ufumbuzi mapema kwa niaba yao ikiwa watafumbua matumizi ya maudhui sanisi au yaliyobadilishwa kwenye kichwa au maelezo ya video zao.

Kinachotokea baada ya watayarishi kufumbua

Watayarishi wakichagua “Ndiyo” ili kuashiria kuwa maudhui yao ni sanisi au yamebadilishwa, tutaweka lebo kwenye sehemu ya maelezo ya video zao. Lebo hizi zitaonekana kwa watazamaji wanaotazama video za YouTube kwenye vifaa vya mkononi au vishikwambi kwa sasa.

Lebo kwenye sehemu ya maelezo yaliyopanuliwa

Lebo ya ziada ya maudhui nyeti

Taarifa zenye ubora wa juu na za wakati unaofaa kuhusu uchaguzi, migogoro inayoendelea, majanga ya asili, fedha au afya ni muhimu sana. Aina hizi za taarifa zinaweza kuathiri sana ustawi, usalama wa kifedha au usalama wa watu na jumuiya. Kwa maudhui kuhusu mada nyeti kama hizi, huenda pia lebo dhahiri zaidi ikaonekana kwenye kicheza video ili kuweka uwazi zaidi.

Athari nyingine za ufumbuzi

Kufumbua maudhui kuwa ni sanisi au yamebadilishwa hakutazuia hadhira ya video au kuathiri hali yake ya kutimiza masharti ya kuchuma mapato.

Hatari za kutofanya ufumbuzi

Inaweza kupotosha ikiwa watazamaji wanafikiri kuwa video ni halisi, wakati imebadilishwa kwa kiasi kikubwa au imezalishwa kwa njia ya usanisi ili ionekane kuwa ni halisi.

Katika hali fulani, maudhui yasipofumbuliwa, huenda YouTube ikachukua hatua ili kupunguza hatari ya madhara kwa watumiaji kwa kuweka lebo ambayo watayarishi hawatakuwa na chaguo la kuiondoa. Pia, watayarishi ambao mara kwa mara wanachagua kutofumbua maelezo haya wanaweza kukabiliwa na adhabu kutoka YouTube, ikijumuisha kuondolewa kwa maudhui au kuondolewa kwa muda kwenye Mpango wa Washirika wa YouTube.

Kumbuka, tunatumia Mwongozo wetu wa Jumuiya kwenye maudhui yote katika YouTube, bila kujali ikiwa ni sanisi au yamebadilishwa.

Je, maelezo haya yamekufaa?

Tunawezaje kuboresha?

Je, unahitaji usaidizi mwingine?

Jaribu hatua zifuatazo:

Tafuta
Futa utafutaji
Funga kisanduku cha kutafutia
Programu za Google
Menyu kuu